TAASISI YA JTFE YAMWAGA VYANDARUA KITUO CHA WATOTO WENYE UALBINO SHINYANGA
Katika
kukabiliana na ugonjwa wa Malaria,Taasisi ya Kimataifa ya Josephat
Torner Foundation Europe (JTFE) inayojishughulisha na masuala ya watu
wenye Ualbino yenye makao makuu yake nchini Uholanzi imetoa msaada wa
vyandarua 50 kwa ajili ya watoto wenye ualbino wanaolelewa katika kituo
cha Buhangija Manispaa ya Shinyanga.
Msaada huo umetolewa na mwenyekiti wa
JTFE, Pieter Staadegaard siku moja tu baada ya kutembelea kituo hicho na
kuelezwa kuhusu upungufu wa vyandarua katika kituo hicho ambapo sasa
kina watoto 228 kati yao wenye ualbino ni 142.
Akikabidhi vyandarua hivyo leo Jumamosi
May 27,2017 Staadegaard alisema vitasaidia kupiga vita ugonjwa wa
malaria na kwamba miongoni mwa malengo ya taasisi hiyo ni kuongeza elimu
kwa jamii kuhusu masuala ya ualbino na kuwawezesha kiuchumi watu wenye
ualbino.
"Nilifikika katika kituo hiki jana May
26,2017 kisha kutoa msaada wa vifaa vya michezo kwa watoto ikiwemo
midoli,miwani ya kuzuia mionzi ya jua lakini pia viatu,nilipomaliza
kugawa zawadi hizo viongozi wa kituo hiki wakaniambia pia kuna upungufu
wa vyandarua,ndiyo nimeamua kuleta vyandarua ili watoto hawa wasije
kupata ugonjwa wa malaria kwa kukosa vyandarua",alieleza Staadegaard.
“Taasisi hii yenye makao makuu yake nchini Uholanzi imeanzishwa mwezi
Januari mwaka 2017 baada ya mimi kukutana na bwana Josephat Torner
mkoani Geita kisha kujadili namna ya kushughulikia masuala mbalimbali
yanayohusu watu wenye ualbino”,aliongeza Staadegaard.
Katika hatua nyingine alisema taasisi hiyo ina mpango kwa kuanza kununua
Kahawa inayozalishwa nchini Tanzania na kuipeleka nje ya nchi kwa lengo
la kuwainua kiuchumi watu wenye ualbino.
Naye Afisa Habari na Uhusiano kutoka Chama Cha Watu Wenye Ualbino nchini
Tanzania (TAS),Josephat Torner alisema katika kuadhimisha siku ya
Albino duniani June 13 mwaka huu,TAS inaendelea kutoa elimu kwa jamii
kuhusu masuala ya ualbino.
Kwa Upande wake Mwalimu mkuu wa Shule ya msingi Buhangija na msimamizi
wa kituo hicho,Seleman Kipanya alishukuru kupokea msaada huo na kuwaomba
wadau kuendelea kujitokeza kusaidia watoto hao.
Mwenyekiti wa Taasisi ya Kimataifa ya Josephat Torner Foundation Europe
(JTFE),Pieter Staadegaard akizungumza katika kituo cha kulelea watoto
wenye ualbino cha Buhangija katika manispaa ya Shinyanga
Watoto wanaolelewa katika kituo cha Buhangija
Afisa Habari na Uhusiano kutoka Chama Cha Watu Wenye Ualbino nchini
Tanzania (TAS),Josephat Torner akizungumza katika kituo cha Buhangija
Afisa Habari na Uhusiano kutoka Chama Cha Watu Wenye Ualbino nchini
Tanzania (TAS),Josephat Torner akizungumza kabla ya kuanza kugawa
vyandarua
Vyandarua vilivyotolewa na Taasisi ya Kimataifa ya Josephat Torner Foundation Europe (JTFE)
Mwenyekiti wa Taasisi ya Kimataifa ya Josephat Torner Foundation Europe (JTFE),Pieter Staadegaard akigawa vyandarua kwa watoto
Afisa Habari na Uhusiano kutoka Chama Cha Watu Wenye Ualbino nchini
Tanzania (TAS),Josephat Torner akiwaelekeza watoto wakati wa kugawa
vyandarua
Zoezi la kugawa vyandarua linaendelea
Afisa Habari na Uhusiano kutoka Chama Cha Watu Wenye Ualbino nchini Tanzania (TAS),Josephat Torner akigawa vyandarua
Msimamizi wa kituo cha Buhangija/Mwalimu mkuu wa shule ya Msingi
Buhangija Seleman Kipanya akitoa shukrani baada ya kupokea msaada wa
vyandarua
Mjumbe wa kamati ya shule ya msingi Buhangija Kuluthum Ally akitoa
shukrani kwa taasisi ya JTFE kutoa misaada katika kituo cha Buhangija.
Picha zote na Kadama Malunde-Malunde1 blog