Uongozi wa Yanga
unatarajia kumuweka kitimoto mshambuliaji wake, Donald Ngoma raia wa
Zimbabwe kumjadili kutokana na vitendo anavyovifanya ndani ya timu hiyo
ikiwemo ya kuondoka na kugomea kuichezea timu hiyo kwa kisingizio cha
kuwa majeruhi.
Ngoma aliyetua
Yanga misimu miwili nyuma, kwa msimu huu amekuwa na msaada kidogo ndani
ya timu hiyo kutokana na kutocheza mara kwa mara kwa sababu ya majeraha
ya goti ambalo limemfanya akose michezo mingi ya timu hiyo.
Katibu wa timu
hiyo, Boniface Mkwasa, alisema wataongea kwa kina na mshambuliaji huyo
juu ya safari yake ya Afrika Kusini alipoenda kutibiwa ambapo alizidisha
siku ambazo alipewa ruksa ya kukaa huko.
“Tunatarajia kuwa
na kikao na Ngoma kutokana na mwenendo wake kwa msimu huu ambapo amekuwa
akikaidi baadhi ya vitu ambavyo tunakubaliana ikiwemo juu ya safari
yake ya Afrika Kusini aliyoenda hivi karibuni.
“Tulimpa ruhusa ya
kwenda kutibiwa huko ili akamalize tatizo lake la goti ambalo
linamsumbua lakini yeye alipitisha siku ambazo tulimpa ruhusa na
kuendelea kukaa huko bila ya idhini yetu na bila ya kuuambia uongozi
lolote lile.
“Sasa tunataka
tumbane kwa ajili ya kujua nini kilichotokea maana ilisemekana kuwa
alifanya mazungumzo na baadhi ya timu hivyo tunataka kujua kama ni kweli
au la,” alisema Mkwasa.
SOURCE: CHAMPIONI