Na Saleh Ally
MWENYEKITI
wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zacharia Hans Poppe ameamua kuachia
ngazi katika nafasi hiyo na sasa atabaki kuwa mwanachama wa kawaida.
Mohammed
Dewji ‘Mo’ ambaye amewahi kuwa mdhamini, mfadhili na hivi karibuni
alitangaza kuingia katika mabadiliko kwa kutaka kununua hisa asilimia 51
za Klabu ya Simba, naye ameamua kukaa pembeni.
Kwa hali inavyokwenda, maana yake tunaweza kusikia na wengine tena wakiwa wamejiondoa katika uongozi au vinginevyo.
Wote
hawa wawili wamekasirishwa na mchakato wa namna Kampuni ya SportPesa
ilivyoingia mkataba na klabu yao jambo ambalo wanaona hawakutendewa haki
na viongozi.
Kila
mmoja anavyozungumza anaonyesha amekerwa na namna ambavyo mchakato
ulipelekwa. Namna mambo yalivyokwenda na inaonekana viongozi walifanya
siri hata dhidi ya viongozi wenzao.
Ukiwaangalia
Mo na Hans Poppe utagundua kitu ambacho huenda hata wewe au mimi
kingeweza kuwa kina uwezo wa kukukuta kama jambo hilo lingekutokea.
Wakati
wa shida, watu walikufuata na kukuchukulia kama sehemu yao, mwokozi,
mshauri na mpiganaji wao, lakini inapofikia wamepata neema, basi wanaona
wewe si mwenzao tena.
Hans
Poppe na Mo Dewji wanaamini wangeweza kuwashawishi SportPesa kutoa
fedha nyingi zaidi za udhamini kuliko ambazo klabu imepata.
Inaonekana
Rais Evans Aveva na wenzake wameamua kufanya mambo haraka kama walikuwa
wanawakimbia wenzao, hawakutaka kuulizwa au walifanya hivyo kwa manufaa
yao au wana faida ya pembeni.
Uamuzi
waliouchukua Mo Dewji na Hans Poppe kujiweka kando. Wana haki kwa kuwa
nao ni binadamu na wanastahili kufanya hivyo kwa mujibu wa hisia zao.
Kuna
mambo kadhaa ya kufikiria, kujitoa kusaidia Simba huku ukibaki kuwa
mwanachama nayo pia inaweza isisaidie sana. Vizuri kuwe na busara ya
kulimaliza jambo hilo kwa njia za kujenga zaidi kuliko kujitenga.
Hakika
ninawaelewa Hans Poppe na Mo Dewji, wanaona kuna hisia za usaliti kwa
kuwa wamewekwa kando hasa baada ya wahusika kuona ni wakati wa neema
tena, neema ambayo wawili hao wanaamini ingekuwa kubwa zaidi kama
wangeshirikishwa.
Kwa
nini Aveva na wenzake waliwakimbia wengine na Simba ikagawanyika wakati
ndiyo inakwenda kupata neema? Hakika ni jambo la kujiuliza, kutafakari
na mwisho kuamini kweli kuna tatizo ambalo linatakiwa kufanyiwa kazi.
Hakuna anayeweza kumaliza matatizo ya Wanasimba isipokuwa ni Wanasimba wenyewe. Wanasimba ni pamoja na Mo Dewji na Hans Poppe.
Hakuna
anayeweza kukataa kuwa Hans Poppe na Mo Dewji wamekosewa. Nafikiri ni
hisia za kijeuri tu, zinaweza kupinga hili kwa kuamini hakuna
kinachoshindikana hata fulani akiondoka kwa kuwa Simba ni kubwa.
Ukubwa
wa Simba unatengenezwa na watu wenyewe ambao ndiyo akina Aveva, Mo
Dewji, Hans Poppe na wengine. Raha zaidi ni watu wenye makampuni
makubwa, maana yake wanaongoza watu wengi tayari.
Hivyo
ni vizuri Simba kuwatumia na hasa kunapokuwa na mambo makubwa kama hayo
kuliko kushirikisha watu ambao huenda wakawa si wazuri katika masuala
yanayohusiana na ushindani wa soko kwa maana ya uendeshaji wa mambo.
Hans Poppe akikaa kando kama Mo Dewji, mwisho watakuwa wanaiumiza Simba na Wanasimba ambao wanawategemea kama askari wao.
Wamekosewa, waliowakosea wawe waungwana na kuzungumza maneno stahili na ikiwezekana kuwashawishi warejee.
Mo
Dewji na Hans Poppe hakuna ambaye ameonyesha anaipinga SportPesa.
Badala yake kila mmoja amechukizwa na mchakato ulioendeshwa na viongozi
wenzake ambao anaona haukuwa uliijenga uaminifu na uwazi na badala yake
uficho wa mambo tu.
Vizuri wakaonyesha busara, wakae pamoja na kulimaliza ili kuthibitisha ile kauli mbiu ya klabu ya “Simba Nguvu Moja.”