TUNAPOSHINDWA KUHISIANA NA TUZO ZA LIGI KUU BARA, NI SEHEMU NDOGO SANA
Na Saleh Ally
TUZO za Ligi Kuu Bara zimekamilika na
kuonyesha kuna mabadiliko kupitia kamati ya tuzo ambayo mara nyingi
imekuwa ikitengeneza malalamiko mengi sana.
Wachezaji, waamuzi na makocha
walioshiriki Ligi Kuu Bara msimu uliomalizika wiki iliyopita wameitwa na
kutuzwa baada ya kujumuika pamoja.
Kawaida, malalamiko ni jambo la kawaida
kunapokuwa na ushindani wa jambo lakini unaweza kupima usahihi wa
unachokifanya kulingana na wingi wa malalamiko yenyewe.
Msimu wa 2016-17, inaonekana kabisa
kwamba hakukuwa na malalamiko mengi kwa kuwa kamati ya tuzo chini ya
Alhaji, Msafiri Mgoyi imeonekana kufanya kazi yake vizuri zaidi
kiweledi.
Malalamiko yanapopungua, maana yake
kunakuwa na umakini umeongezeka. Hii inaonyesha kamati imejifunza
kutokana na makosa yaliyotokea huko nyuma kulingana na hali halisi.
Hili ni jambo jema la kusifia, lakini bado inaonekana kuna mambo madogo yamekuwa yakiendelea kila tuzo hizo zinapofanyika.
Mfano pale ukumbini, maandalizi
yanaonekana kutoboreka katika kiwango ambacho kinaonekana vitu vimepiga
hatua na hasa katika suala la uwasilishaji.
Kwa kuwa tuzo hizo zinaonyeshwa moja kwa
moja na runinga, ni lazima kulenga ile hali kuwa ile ni shoo sahihi
ambayo inapaswa kuonekana katika mpangilio bora kabisa.
Hakuna chenye ugumu kwa kuwa mambo mengi
ni ya kawaida kabisa na kama ni suala la mabadiliko basi ni kidogo
yanaweza kubadilishwa na kuwa mambo bora kabisa.
Mfano, anapoitwa mtu kwenda kukabidhi
tuzo, anatajwa jina, anaanza kupanda pale juu akitokea sehemu waliyokaa
watu. Baada ya hapo, aliyeshinda naye anapanda. Hili ni jambo la
kizamani na lilishapitwa na wakati. Tunajua kuwa washindi na wanaotakiwa
kukabidhi hutokea “back stage”. Wanafika pale mbele na baada ya
kukabidhi na kupokea, wanarudi tena nyuma ya jukwaa.
Maana yake, wanapaswa kuandaliwa mapema
na kuwa nyuma ya jukwaa. Akiitwa fulani kukabidhisha anatokea nyuma ya
jukwaa. Baada ya hapo anayekwenda kukabidhiwa naye anafuatia.
Unapozungumzia zile picha za video za
wachezaji mbalimbali zilipokuwa zinaonyeshwa, nyingi zinaonekana
hazikuandaliwa vya kutosha na mfano mzuri ni ile ya beki wa Simba,
Mohamed Hussein Zimbwe maarufu kama Tshabalala.
Ndiye mchezaji bora, lakini haikuwa
imeandaliwa wala hakuwa ikionyesha hata mambo muhimu matatu aliyoyafanya
uwanjani zaidi ya kona aliyopiga, hiki ni kichekesho.
Kuna suala la shukurani ambalo linaweza
kurekodiwa kwa dakika moja. Mchezaji akafuatwa hata kwake na kuzungumza
jambo ambalo watu walio ukumbini na wanaoangalia mubashara nao
wakashuhudia vizuri.
Jiulize, Azam TV ndiyo wadhamini wa ligi
kuu, wana wataalamu kibao wa kutengeneza mambo mazuri na picha za video
wanazo kwa kuwa wameonyesha mechi nyingi mubashara. Sasa tatizo nini
kila kitu kinazidi kuonekana hakina maandalizi bora wakati wa shoo kubwa
kama hiyo.
Wachezaji wakongwe, utamuona mtangazaji
katika hafla hiyo akijaribu kuwazungumzia. Si kwa kina kwa kuwa ana
mambo mengi yanamwandama. Iko wapi shida kukiwa na picha fupi angalau
dakika moja na nusu ikimzungumzia Kitwana Manara au Sunday Manara kwa
msaada wake mwenyewe na watu wakatulia wakishuhudia kabla ya yeye
mwenyewe hajatokea jukwaani.
Kweli kuna kujifunza na hilo ni jambo
jema. Inaonekana tunapokwama ni sehemu ambayo haina hata ugumu wa
kung’oka. Mazoea na kwa kuwa waandaaji huenda wanaona mambo yanakwenda,
basi hawawezi kujali.
Kizuri ni gharama na hii haina maana ya
gharama kwa fedha tu, unaweza kugharamia jambo kwa kutumia muda na akili
yako na kufanya kitu bomba maradufu.
Ningependa kuchangia hivi, kwamba msimu
ujao, basi kuna haja ya kufanya kitu kizuri zaidi ambacho pia kinatoa
nafasi kubwa ya shukurani kwa wadhamini ili kuwashawishi na wajione wako
katika mikono salama.