SERIKALI YA TANZANIA YAMPATIA MATIBABU MZEE ALIYECHORA NEMBO YA TAIFA
Serikali ya imelazimika kumuhamishia katika Hospitali ya Taifa ya
Muhimbili Mzee Francis Maige Ngosha aliyekuwa amelazwa katika Hospitali
ya Amana kwa kipindi cha siku moja kwa ajili ya kupatiwa matibabu zaidi.
Akitoa tamko la serikali Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya jamii,
Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Khamisi Kigwangalla amesema mzee huyo
ambaye ni mmoja wa wachora Nembo ya Taifa amesema wameamua kumuhamishia
katika hospital hiyo ya Taifa Muhimbili ili kufanyiwa uchunguzi wa kina
na wataalamu wa magonjwa mbalimbali ili kubaini na kutibiwa.
Dkt. Kigwangalla amesema serikali itahakikisha inampa tiba kamili na
malezi kwa kuzingatia haki ya kuishi ya binadamu na kuthamini mchango wa
wazee na waasisi wa taifa.
Kwa upande wake daktari bingwa wa magonjwa ya dharura kutoka Hospitali
ya Taifa ya Muhimbili Dkt. Juma Mfinanga amesema wanasubiri majibu ya
vipimo wanavyomchunguza na pindi watakapobaini tatizo atapatiwa matibabu
yake.
Kwa upande wake Francis Maige Ngosha ambaye ni mmoja wa wachora Nembo ya
Taifa ameishukuru serikali na jami iliyokuwa ikimlea kwa miaka yote
bila malipo.