ACACIA WAPINGA UCHUNGUZI WA KAMATI YA RAIS MAGUFULI,MKUU WA MKOA WA SHINYANGA ATUA KWENYE MIGODI
VITA
kubwa. Ndivyo unavyoweza kusema baada ya Rais Dk. John Magufuli kuanza
kuchukua hatua kali dhidi ya usafirishaji wa mchanga unaodaiwa kuwa na
dhahabu.
Baada ya hatua hiyo ya Rais Magufuli,
kumeanza kuibuka mambo kadhaa, moja kubwa likiwa ni msafara wa Kamati ya
Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Shinyanga ukiongozwa na Mkuu wa Mkoa,
Zainab Tellack kuzuiwa kuingia kukagua na kuhesabu dhahabu iliyozalishwa
na mgodi wa dhahabu wa Bulyanhulu kwa kipindi cha siku mbili, baada ya
Wakala wa Ukaguzi wa Madini (TMAA) kusimamishwa.
Zainabu, alikuwa katika ziara ya kawaida
kukagua wingi za dhahabu iliyozalishwa katika migodi iliyopo mkoani
kwake, baada ya Rais Magufuli kusimamisha kazi watendaji wa TMAA.
Akizungumza na waandishi wa habari jana,
Zainabu alisema kutokana na TMAA kuondolewa, waliamua kufanya ukaguzi
migodini kujua ni nini kipo na kimezalishwa wakati ili kuhakikisha
usalama wa madini hayo.
Alisema alichukua uamuzi huo kuepuka udanganyifu hadi wataalamu wengine watakapopatikana kwa kazi ya ukaguzi.
“Tulifanikiwa kufika mgodi wa Buzwagi,
tulikagua na kupima kiasi cha dhahabu kilichokuwapo na kuhesabu…
tulipofika mgodi wa Bulyanhulu tuliingia ila hatukufunguliwa strong room
(chumba cha kuhifadhia dhahabu) kama Buzwagi kwa madai wanafunga kwa
muda (time lock), tulikubaliana kesho (leo), lakini nimeamua kuweka
askari wa kulinda hapo mpaka kesho (leo),” alisema.
Alisema hawezi kuacha wawekezaji hao
wakazalisha dhahabu bila ya kuwa na wakaguzi kama taratibu
zinavyoelekeza, kwa kuwa wanaweza kuzalisha na kusafirisha wakati ambao
hakuna wakaguzi.
“Labda niwaambie Watanzania, dhahabu
yetu ipo salama, tumekagua na kujihakikishia walichozalisha kwa kuhesabu
na kupima, waliposema hatuwezi kuingia, nimeweka ulinzi wa Serikali,”
alisema.
ACACIA WAFAFANUA
Meneja Mawasiliano wa Kampuni ya Acacia
ambayo ndiyo wamiliki wa mgodi wa dhahabu wa Bulyanhulu, Nekta Foya,
akizungumza na MTANZANIA jana, alisema Mkuu wa Mkoa alifika na kupokewa
vyema katika mgodi wa Bulyanhulu na kupewa ushirikiano wote hadi kuingia
ndani ya chumba cha dhahabu (gold room), lakini hakuingia katika sefu
ya dhahabu kutokana na muda aliofika kuwa imejifunga.
“Unajua kwa ajili ya usalama, unaweza
kuingia chumba cha dhahabu, usifike kwenye dhahabu kwa kuwa hufungwa kwa
muda maalumu kutokana na mipango ya uzalishaji, sasa muda ambao amefika
mfumo wetu wa usalama (time lock) wa sefu ya dhahabu, ulikuwa
umejifunga, usingeweza kufunguka hadi kesho (leo),” alisema.
Alisema baada ya kufahamishwa na maofisa
wao waliokuwapo, RC Zainabu alikubalina nao na kupanga kuendelea kesho
na ukaguzi wake, lakini kutokana na kutaka uhakika zaidi aliacha askari
kulinda eneo hilo.
YAPINGA RIPOTI YA KAMATI
Katika hatua nyingine, Acacia imepinga
ripoti ya Kamati ya Profesa Abdulkarim Mruma iliyoundwa na Rais,
Magufuli kuchunguza makontena 277 yenye mchanga wa dhahabu, ikisema
haikutangaza madini yote yaliyokuwa katika makanikia inayosafirisha
kwenda nje ya nchi.
Ikumbukwe Rais Magufuli aliunda kamati
mbili kuchunguza kiwango cha madini kilichomo katika makontena hayo ya
mchanga yaliyokuwa yakisafirishwa kwenda nje ya nchi kuyeyushwa kupata
masalia baada ya mchakato wa kwanza kuondoa dhahabu mgodini.
Kamati hiyo iliyokabidhi ripoti yake
Ikulu juzi iliongozwa na Profesa Abdulkarim Mruma ambaye alisema
makontena yaliyozuiwa katika Bandari ya Dar es Salaam yana tani 7.8 za
dhahabu yenye thamani ya kati ya Sh bilioni 676 na Sh trilioni 1. 147.
Katika taarifa yake kwa vyombo vya
habari Dar es Salaam jana, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Acacia,
Brad Gordon, alisema kamati hiyo haikutangaza madini yote yaliyokuwa
katika makanikia kwamba kutokana na hilo, amri ya kuyazuia kusafirishwa
nje kubakia palepale.
“Hatukubaliani
na matokeo ya tume ambayo inaeleza kuwa madini yaliyo katika mchanga
uliopo katika makontena yana thamani zaidi ya mara 10 ya kiwango
tulichotangaza.
“Tuna imani na usahihi wa taarifa zetu
ambazo zilikaguliwa na kutathiminiwa na SGS, ambayo ni moja ya kampuni
kubwa kabisa duniani za upimaji,”alisema Gordon.
Ofisa huyo wa Acacia, alisema makanikia
wanayozalisha yana kiwango kidogo cha madini na kila kontena lina
kiwango tofauti cha wingi wa makanikia, lakini wanaamini kila kontena
lina wastani wa kilo 3,000 za shaba, tatu za dhahabu na kilo tatu za
fedha.
Alisema kwa pamoja madini hayo yana thamani ya Sh milioni 300 kwa kila kontena.
“Pia tumeorodhesha kampuni huku mapato
yetu yakikaguliwa kikamilifu na PWC, ambayo inathibitisha kwamba daima
tuko wazi kwa kila kitu tunachofanya.
“Mapato tunayotangaza katika mahesabu yetu yaliyokaguliwa yanaendana na kiwango cha dhahabu tunachotangaza kuzalisha na kuuza.
“Iwapo kiwango cha dhahabu katika
makanikia yetu kitaendana na matokeo ya tume, itamaanisha kwamba migodi
ya Bulyanhulu na Buzwagi inazalisha dhahabu nyingi kuliko mgodi wowote
ule duniani. Kwa bahati mbaya sana uhalisia hauko hivyo.
“Nakubali kwamba wakati matukio kama ya
jana yanapotokea, huleta hali ya sintofahamu na kuwafanya watu wahoji na
wamwamini nani. Nataka kuwahakikishia kwamba Acacia ilitangaza
kikamilifu kila kitu kwa mujibu wa thamani halisi tunayozalisha.
“Pia tunalipa mirabaha inayotakiwa na
kodi kwa madini yote yanayohusika ambayo tunazalisha na kwamba
usafirishaji wa makanikia hufanyika kwa mujibu wa sheria za Tanzania na
makubaliano ya kisheria tuliyonayo na Serikali ya Tanzania.
“Wakati tukiwa tumesikiliza hotuba za
jana (juzi) na taarifa kwa vyombo vya habari ni hadi pale tutakapopokea
ripoti nzima vinginevyo ni vigumu kwetu kutoa maelezo ya kina au kutoa
uamuzi kuhusu kiwango na thamani inayohusu makanikia ya Acacia kwa
mujibu wa ripoti ya tume, lakini ninarudia, tunaamini juu ya kiwango
tulichotangaza.
“Kuhusu mirabaha alisema Serikali
hupokea mirabaha ya asilimia nne ya madini ya dhahabu, fedha na shaba
iliyopo katika makanikia.
“Acacia imekuwa ikilipa mirabaha na kuna
ukaguzi wa kuthibitisha hilo. Madini mengine katika makanikia hayo ni
yale yasiyo na thamani katika soko kutokana na kiwango cha udogo wake na
gharama za kuyachenjua huzidi thamani na hivyo hakuna mrabaha,”alisema
ofisa huyo wa Acacia.
Wakati Kampuni ya Acacia ikisema hivyo,
timu ya Wanasheria Watetezi wa Mazingira kwa Vitendo (LEAT), ilitoa
mapendekezo kadhaa kwa Serikali huku ikiitaka kuzidai kampuni zote
malimbikizo ya kodi na mrabaha wa madini ambayo hazikuyataja katika
taarifa zao tangu zilipoanza uchimbaji hapa nchini.
Taarifa hiyo pamoja na mambo mengine
imependekeza Katiba ya nchi ifanyiwe marekebisho na kutamka wazi kuwa
Tanzania ndiyo mmiliki wa milele wa rasilimali zake zote za asili.
Mkurugenzi Mtendaji wa LEAT, Dk.
Rugemeleza Nshala, alisema kuna mfumo mbaya wa ukaguzi na mikataba ya
madini ambao unaruhusu kampuni kushiriki katika udanganyifu wa bei.
“Serikali ifute leseni za uchimbaji kwa
kampuni za madini ambazo zimeshiriki katika udanganyifu huu. Tunatoa rai
kwa Serikali hatua zote za kisheria za kuvunja mikataba zifuatwe kwani
uzoefu wetu katika kesi ya City Water unatuasa kufuata kwa umakini
taratibu za kuvunja au kusitisha mikataba.
“Iundwe idara madhubuti ya wanasheria
ndani ya Serikali wanaohusika na masuala ya gesi, petroli, madini na
mikataba yote ipitiwe kuona udhaifu wake,” alisema Dk Nshala.
Aidha LEAT inaishauri Serikali kushiriki
katika uchimbaji wa madini kupitia kampuni zake na iwe na hisa katika
kampuni mama zinazochimba madini huku ikitolea mfano nchi ya Botswana
ambayo ilikuwa na asilimia 15 ya hisa katika kampuni ya ubia kati yake
na De Beers.
Dk. Nshala alisema Tanzania inapaswa
ijitoe katika mikataba ya usuluhishi na migogoro ya kimataifa kwani
inapingana na maazimio namba 1803 ya mwaka 1962 na namba 3281 ya mwaka
1974.
Alisema migogoro yote inayohusiana na
uchimbaji madini kati ya serikali na kampuni za nje za madini
itatatuliwa na mahakama za ndani na si mabaraza ya usuluhishi kwa madai
kuwa yalianzishwa kulinda masilahi ya kampuni za kigeni.
Kuhusu kodi, mwanasheria huyo
alipendekeza sheria ya kodi irekebishwe na kuweka vifungu vya kuzuia
udanganyifu wa bei na kufuta nafuu zote za uwekezaji za uchimbaji madini
zilizo katika sheria ya mabadiliko ya sheria mbalimbali za fedha namba
27 ya mwaka 1997 na sheria ya mauzo ya mwaka 1976 kwani zimebariki
kuporwa kwa madini.
“Yale ambayo kamati imeyabaini ni mambo
ambayo LEAT ilikuwa ikiyasema kwa sauti kubwa lakini yalipokelewa kwa
kejeli na uongozi wa Serikali zilizopita zikiungwa mkono na kampuni za
madini kwa kuwaita wanaharakati wenye ajenda ya siri dhidi ya
wawekezaji,” alisema.
Kwa mujibu wa mkurugenzi huyo baada ya
malalamiko ya wadau, Benki ya Dunia iliikopesha Serikaliya Tanzania Dola
za Marekani milioni 56 kufanya mabadiliko katika Sheria ya Madini ya
1998 na kuandikwa sheria nyingine mwaka 2010.
Alisema sheria hiyo ya 2010 haina
tofauti na ile ya 1998 isipokuwa kuanzishwa kwa bodi ya ushauri ya
madini na waziri kuchukua nafasi ya kamati ya ushauri na kushauri
ipitiwe upya.
PROFESA MOSHI
Mhadhiri wa Uchumi katika Chuo Kikuu cha
Dar es Salaam (UDSM), Profesa Humphrey Moshi, akitoa maoni yake jana
alisema kosa kubwa lililofanywa na Serikali ni kufungua milango ya
wawekezaji katika sekta ya madini bila kuwa na uwezo wa kuwadhibiti.
“Nilitarajia ripoti itaonesha matokeo
hayo na hili nililizungumza tangu mwaka 2002, kwamba mikataba mingi
haipo wazi hivyo ni rahisi sana kuwa na makandokando.
“Tulifungua milango ya kukaribisha
wawekezaji bila hata kuwa na uwezo wa kuwadhibiti, hili ni kosa kubwa.
Wawekezaji walipewa masharti ambayo ni nafuu mno. Serikali ikutane na
wawekezaji wote na wakubaliane kwamba lazima mikataba ipitiwe upya,”
alisema Profesa Moshi.
PROFESA SHIVJI
Mhadhiri Mstaafu wa Chuo Kikuu cha Dar
es Salaam (UDSM), Profesa Issa Shivji, aliandika katika ukurasa wake wa
Twitter jana akisema Serikali ilikosa njia ilipopitisha sheria ya madini
mwaka 1998.
“Tulikosa njia tulipopitisha sheria ya
madini ya mwaka 1998 iliyofanya mikataba iwe na nguvu zaidi kuliko
sheria. Tukajifunga pingu. Nani wa kulaumu?,” alihoji Profesa Shivji.
LHRC
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha
Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Anna Henga, alisema mwaka 2014,
walitoa ripoti na kuiomba Serikali ichungunze na kuichukulia hatua
Wakala wa Madini Tanzania (TMAA), lakini hawakusikilizwa.
“Tumeridhishwa na hatua zilizochukuliwa
japo ni kwa kuchelewa. Mwaka 2014 tulitoa ripoti yetu na maoni yetu
kuhusu mikataba ya madini na tukaiomba Serikali iichunguze TMAA lakini
hawakutusikiliza ni wakati sasa wa kupitia upya mikataba yote ya
madini,”alisema Henga.
CCM: Rais akaze buti
KATIBU wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha
Mapinduzi(CCM), Humphrey Polepole alisema kwamba Rais Magufuli anapaswa
kuungwa mkono kwa sababu vita hii ya uchumi aliyoingia ni ngumu kuliko
ile ya kutumia silaha.
Watanzania kwa pamoja wanapaswa kuungana
ili kuhakikisha kuwa viongozi au watu wanaohujumu uchumi wa nchi
wanakomeshwa na kuchukuliwa hatua.
Wakati huo huo Umoja wa Vijana wa chama
hicho (UVCCM) umeishauri serikali kupitia upya mikataba yote ya madini
ili kubaini kama ina manufaa kwa taifa ama laa.
Kaimu Katibu Mkuu wa UVCCM, Shaka Hamdu
Shaka wakati akitoa tamko la umoja huo jana alisema pamoja na jitihada
zinazofanywa na Rais Magufuli kuzuia utoroshaji wa madini lakini pia
kama kuna viongozi waliohusika wachunguzwe mali zao na ikibidi
zitaifishwe.
“Tumeishauri serikali kutaifisha mali za
viongozi na watendaji ambao watabainika kumiliki mali, utajiri, na
vitega uchumi ambavyo havilingani na vipato vyao kama ilivyofanyika
mwaka 1967 baada ya kutangazwa kwa Azimio la Arusha ,” alisema Shaka.
Habari hii imeandaliwa na Elizabeth Hombo, Nora Damian, Patricia Kimelemeta na Tunu Nasssor.
Chanzo-MTANZANIA