LIGI KUU BARA IMEISHA UPANDE WA UWANJANI, SIMBA WAAMUA KUHAMIA DODOMA
Baada ya kuukosa ubingwa wa ligi, benchi
la ufundi la Simba chini ya kocha wake, Joseph Omog, raia wa Cameroon,
limeweka wazi kuwa litajipoza machungu yake kwa kuifunga Mbao kwenye
mechi ya fainali ya Kombe la Shirikisho (FA) ili kujipatia nafasi ya
kushiriki michuano ya kimataifa mwakani.
Omog na Simba yake walishuhudia
wapinzani wao wakuu Yanga wakichukua ubingwa wa ligi kwa msimu huu licha
ya wote kuwa na pointi 68, lakini wapinzani wao hao wamewapita kwa
idadi ya mabao ya kufunga na kufungwa.
Mcameroon huyo ameliambia gazeti hili
kuwa, hawajakata tamaa juu ya kikosi chao kutwaa ubingwa katika msimu
huu, baada ya kuikosa ligi kwani sasa ameelekeza ujuzi wake kuhakikisha
anaisaidia timu hiyo kuchukua FA.
“Kila mmoja ameona jinsi ambavyo
tulipambana tangu mwanzo wa ligi mpaka mwisho wake ambapo tumekosa
ubingwa kwa tofauti ya mabao pekee, lakini nia yetu ilikuwa ni kuutwaa
ubingwa ili tujikatie nafasi ya kushiriki michuano ya kimataifa.
“Lakini hiyo siyo kitu kwa sababu licha
ya kukosa kwa njia hiyo ya kuchukua ligi, kwa sasa tuna mechi ya fainali
mkononi ambayo hiyo tunataka kuitumia kwa ajili ya kupoza machungu yetu
ya kukosa ubingwa lakini pia kujipatia nafasi ya kushiriki michuano ya
kimataifa ambapo mara ya mwisho ilikuwa miaka mitano nyuma,” alisema
kocha huyo.