MKATABA WAMTIA MAWENGE NDAYIRAGIJE, AONDOKE AU ABAKI MBAO
Kocha
wa Mbao FC, Ettiene Ndayiragije raia wa Burundi, amesema mkataba wake
unamzuia kuanza kufikiria kujiunga na timu nyingine ambazo zinatajwa
kumuwania.
Leo Jumamosi kocha huyo ataiongoza Mbao kucheza fainali ya Kombe la FA dhidi ya Simba kwenye Uwanja wa Jamhuri, Dodoma.
Ndayiragije
ambaye aliwahi kuinoa Vital’O ya nchini kwao, ameyasema hayo huku
kukiwa na tetesi kwamba anatakiwa kwenda kuchukua mikoba ya Mmalawi,
Kinnah Phiri ya kukinoa kikosi cha Mbeya City.
Mrundi huyo amesema kuwa, kutokana na mkataba wake alioingia na Mbao, unamnyima nafasi ya kuanza kupigia hesabu timu nyingine.
“Si
kweli kama nataka kwenda Mbeya City, mimi ni kocha wa Mbao na watu
wanatakiwa kulitambua hilo kwamba sina mpango wa kuondoka sasa hivi.
“Mkataba
wangu na Mbao unanizuia kuanza kufikiria kujiunga na timu nyingine,
inawezekana ipo timu inayonihitaji lakini binafsi sina taarifa hizo na
sijafanya mazungumzo na timu nyingine,” alisema Ndayiragije.
Ikumbukwe
kuwa, kocha huyo alisaini mkataba wa mwaka mmoja ambao unaisha hivi
karibuni, lakini mwenyewe amesisitiza kuna makubaliano ambayo aliingia
na mabosi wake. Makubaliano hayo alidai ni siri yao.
SOURCE: CHAMPIONI