MBEGU BORA ZA MHOGO ZINAHITAJIKA KUWANUSURU WAKULIMA WILAYANI CHATO MKOANI GEITA.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Ipandikilo kilichopo katika Halmshauri ya Wilaya ya Chato, Lazaro Kagundulilo (kulia),
akizungumza na wanahabari pamoja na wataalamu wa kilimo kutoka Tume ya
Taifa ya Sayansi na Teknolojia (Costech) na , Jukwaa la Bioteknojia na
Uhandisi Jeni (OFAB), wilayani humo jana. Wataalamu hao wa kilimo wapo
katika wilaya hiyo kwa ziara ya kutoa mafunzo ya kilimo chenye tija kwa
maofisa ugani wa Mkoa wa Geita.
Maofisa ugani wakiangalia eneo ambalo patalimwa shamba dogo la mfano katika Kijiji cha Kibehe Kata ya Kigongo.
Mtaalamu wa masuala ya mizizi kutoka
Kituo cha Utafiti wa Kilimo cha Ukiliguru jijini Mwanza, Dk. Jeremiah
Simon (kulia), akitoa maelezo kwa wanahabari wakati walipotembelea moja
ya shamba la zao la mhogo lililokumbwa na ugonjwa wa batobato na
michirizi ya kahawia wakati wa ziara hiyo katika Kijiji cha Ipandikilo.
Mwenyekiti wa Kijiji
cha Ipandikilo kilichopo katika Halmshauri ya Wilaya ya Chato, Lazaro
Kagundulilo, akiwaonesha waandishi wa habari shina la mhogo
lililoathiriwa na magonjwa.
Ofisa Program wa OFAB kutoka Shirika la
AATF la nchini Kenya, Suleiman Okoth (kushoto), akiwaelekeza jambo Ofisa
Mtendaji wa Kijiji cha Ipandikilo, Clara Fidelis (kulia) na Ofisa Ugani
wa Wilaya ya Chato, Charles Ntaki.
Shamba la mhogo lililoathiriwa na magonjwa.
Wanahabari wakitoka shambani.
Wakulima wa Kijiji cha Ipandikilo
wakimenya mihogo tayari kwa kuianikwa kwa ajili ya unga wa ugari. Kutoka
kulia ni Veronica Zakaria, Joyce Joseph na Teloza Lugiyege.
Shamba la mhogo linaloonekana kustawi vizuri lakini tayari limeathiriwa na magonjwa ya batobato na mchirizi kahawia.
Mkulima Andrew Misano akitoa maelezo kwa wanahabari kuhusu changamoto mbalimbali za kilimo cha mhogo.
Mtaalamu wa masuala
ya mizizi kutoka Kituo cha Utafiti wa Kilimo cha Ukiliguru jijini
Mwanza, Dk. Jeremiah Simon (kushoto), akizungumza na wakulima wa kijiji
cha Ipandikilo kuhusu mbegu bora za mhogo.
Mjumbe wa Kijiji cha Idoselo, Majeshi Mussa akiwaonesha waandishi wa habari mtama ulioathirika kwa kukosa mvua.
Na Dotto Mwaibale, Chato
MBEGU bora za zao la mhogo
zinazositahimili magonjwa ya Batobato na michirizi kahawia zinahitajika
ili kuweza kunusuru kukumbwa na baa la njaa kwa wakulima wa zao hilo
katika Wilaya ya Chato mkoani Geita baada ya mbegu walizolima msimu huu
kushambuliwa na magonjwa.
Wananchi wa wilaya hiyo wanategemea
zaidi zao la mhogo kama chakula chao kikuu pamoja na biashara lakini
hivi sasa hali siyo shwari kutokana na mihogo waliyopanda kushambuliwa
na magonjwa.
Akizungumza na wataalamu wa kilimo
kutoka Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia na watafiti wa kilimo
kutoka Jukwaa la Bioteknolojia Tanzania (OFAB), walio katika ziara ya
kutoa mafunzo ya kilimo chenye tija wilayani humo leo, mkulima wa zao la
mhogo katika Kijiji cha Ipandikilo, Andrew Misano alisema changamoto
kubwa waliyonayo ni magonjwa yanayoshambulia zao hilo.
Misano alisema msimu wa mwaka huu
umekuwa tofauti na misimu mingine kutokana na zao la mhongo kushambuliwa
na magonjwa ya batobato na michilizi kahawia.
"Msimu huu nimelima ekari saba za mhogo
lakini sitegemei kuvuna chochote kutokana na kushambuliwa na magonjwa
hayo" alisema Misano.
Misano alisema kukosekana kwa mbegu
bora na inayostahimili magonjwa kumechangia wakulima kuwa na changamoto
ya zao hilo katika maeneo mengi ya wilaya hiyo.
Kaimu Ofisa Kilimo na Umwagiliaji wa
Wilaya ya Chato, Faidaya Isango alisema zao la mhogo katika wilaya hiyo
limeshambuliwa na magonjwa kwa zaidi ya asilimia 60 katika Tarafa za
Kechumba, Namilembe na Busilayombo ambapo ameeleza kuwa isipopatikana
njia mbadala ipo hatari ya kuwepo uhaba mkubwa wa chakula.
Alisema changamoto nyingine kubwa
iliyopo ni kwa wakulima kuendelea kung'ang'ania mazao ya mihogo
iliyoshambuliwa na magonjwa badala ya kuing'oa kama wanavyoshauriwa na
maofisa ugani ili isisambaze ugonjwa katika maeneo mengine.
Alisema kunasheria zimeandaliwa kwa
ajili ya kuwabana wakulima wakaidi na zipo katika hatua ya kuanza
kufanya kazi baada ya kupitishwa rasmi.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Ipandikilo
Lazaro Kagundulilo alisema awali katika ekari tatu za mhogo kabla
ugonjwa huo haujaanza walikuwa wakivuna magunia zaidi ya 25 lakini hivi
sasa hawategemei kupata hata magunia matano jambo ambalo ni changamoto
kubwa kwao.
Mtaalamu wa mizizi kutoka Kituo cha
Utafiti wa Kilimo cha Ukiliguru Dk.Jeremiah Simoni alisema njia mbadala
ya kuwasaidia wakulima hao ni kuanzisha mashamba darasa ambayo yataweza
kutoa mbegu safi ambazo hazina magonjwa ya Batobato na michilizi kahawia
kutokana na magonjwa hayo kutokuwa na dawa mbadala.