Kocha
Mkuu wa Simba, Mcameroon, Joseph Omog, amesema kuwa bado malengo yake
hayajatimia licha ya kuwa baada ya kutinga fainali ya Kombe la FA juzi,
ana asilimia kubwa ya kupanda ndege kwenda kushiriki michuano ya
kimataifa mwakani.
Kauli
hiyo, aliitoa mara baada ya timu yake kutangulia kwenye hatua ya
fainali ya Kombe la FA kwa kuwafunga Azam FC bao 1-0 juzi Jumamosi
kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Simba
itakuwa na uhakika zaidi wa kushiriki michuano ya kimataifa kama Yanga
ilifanikiwa kuifunga Mbao FC katika mchezo huo wa FA jana CCM Kirumba,
Mwanza.
Omog amesema malengo yake yeye ni kuhakikisha anaipa Simba makombe yote wanayoshiriki likiwemo la Ligi Kuu Bara na la FA.
Omog
alisema, kikubwa atakachokifanya yeye hivi sasa ni kuhakikisha
anashinda kila mchezo utakaokuwa mbele yake ili kufanikisha malengo
yake.
“Nimeona
mashabiki na viongozi wa Simba wakifurahi kuwatoa Azam katika mechi ya
nusu ya fainali ya FA na kupata uhakika wa kushiriki michuano ya
kimataifa kama Yanga wataifunga Mbao.
"Lakini
kwangu mimi bado sijatimiza malengo yangu niliyojiwekea ya kuchukua
makombe yote tunayoshiriki, la ligi kuu na hili la FA. "Nishawaambia
wachezaji wangu tayari kwa kuwapa tahadhari mapema ya kutoridhika na
hatua hii tuliyofikia na badala yake tunahitaji makombe kama
unavyofahamu muda mrefu Simba haijachukua ubingwa," alisema Omog.