MBEYA CITY NA JEZI YENYE MSALABA BILA YA KUTAFAKARI


Na Saleh Ally

MOJA ya timu ambazo zimekuwa na mpangilio mzuri wa mambo kadhaa yanayohusiana na utawala wa klabu husika ni Mbeya City.


Tumeona mambo mengi ya Klabu ya Mbeya City yamekuwa yakipelekwa kwa utaratibu mzuri ambao unatakiwa kuwa mfano kwa klabu nyingi zikiwemo hata zile kongwe za Yanga na Simba.


Angalia namna ambavyo wamekuwa wakiwatangaza wadhamini wao, mfano jezi mara zote utaona zinatumika wakati wa kusajili wachezaji wapya au kuwatambulisha. Nyuma yao utaona kuna bango lililojaza majina ya wadhamini wao.

Mara karibu zote unapowaona wachezaji wake wakiwa pamoja, basi watakuwa wamevaa sare zao na lazima uone jina la wadhamini wakiwemo wakuu kama betri za RB, Coca Cola na kadhalika. Hii imefanya mara nyingi tuone klabu hiyo ina mpangilio bora.

Nimewahi kuzungumzia kuhusiana na ubora huo wa Mbeya City na nikaeleza kuwa ninaamini kwa kuwa inamilikiwa na Manispaa ya Mbeya, wao kufanya mambo kwa mpangilio si jambo geni kwa kuwa ni ofisi ambayo inaendesha mambo mengi ya Jiji la Mbeya.



Lakini nimeamua kuandika makala haya kuwakumbusha sasa kwamba wanaanza kupotoka na wakiendelea hivi, basi watatumbukia katika shimo ambalo nimekuwa nikilipigia kelele.

Shimo la kufanya mambo kienyeji au kukurupuka bila ya kutafakari mambo ambayo ni sahihi.




Juzi, nimeona Mbeya City wakiingia mkataba na kampuni mpya ya mavazi ambayo nimeelezwa ni ya hapa chini na watakuwa wakivaa jezi hizo sasa.

Wakati wa kuwatambulisha wadhamini hao, niliona jezi za Mbeya City hazikuwa na majina ya wadhamini wakuu betri za magari za RB na wadhamini wengine, jambo ambalo halikuwa sahihi hata kidogo.

Lakini ubunifu au mfumo wa jezi mpya za rangi ya zambarau na nyeupe, zinaonyesha mistari miwili inayopishana  mfano wa msalaba.

Kawaida lazima kujifunza umakini wa timu kuhusisha na masuala ya dini au ukabila. Kwetu Tanzania si jambo sahihi kama ambavyo Hispania Barcelona wanaweza kujihusisha na mambo ya siasa kuhusiana na Catalunya na serikali ya Hispania.




Lakini ukifuatilia kwenye nembo ya Real Madrid, juu utaona msalaba, kwenye nembo ya Barcelona kuna msalaba pia. Hata bendera za nchi kama England, Sweden, Norway, Finland na kadhalika pia zina misalaba na lazima tukubali nchi za wenzetu, zimejipambanua, hii ni nchi ya Kikristo.


Ukienda Uturuki, Algeria, Tunisia utaona wakitumia mwezi, hata katika bendera za nchi zao zinaonyesha, wao ni nchi za Kiislamu. Hili halina tatizo kwao kama kuna timu itaamua kutumia mwezi au msalaba.

Lakini kwetu Tanzania, nchi yetu haina dini. Mashabiki wetu kwenye timu hawana dini. Hivyo si sahihi kuwa na ubunifu au dizaini inayohusisha masuala ya kidini.

Ukiwauliza Mbeya City kwa sasa watakuambia hapana, hii ni “dizaini”, lakini lazima wajifunze kutafakari, kwamba kufanya hivi baadaye nini kitafuatia au athari zake ni zipi.




Wakati mzuri wa kuamua ni ule unaotafakari kabla ya kufanya jambo. Binafsi naona Mbeya City hawakujipanga na hawakulipa kipaumbele hili.


Mbeya City wajifunze, timu yao haina dini na wajifunze kufanya mambo ya kuwakera baadhi hata kama ni wachache si sahihi na kama watakuwa wastaarabu, basi hawapaswi kutumia jezi yenye dalili ya kuonyesha upande fulani wa dini. Haiwezi kuwa sawa.

Kuhusiana na suala la jezi kutokuwa na nembo za wadhamini wanaweza kusema ilikuwa siku ya kumtambulisha mdhamini mpya wa jezi.

Lakini ukweli ni hivi, lazima wadhamini wote wawe pamoja na hasa mdhamini mkuu anatakiwa kupewa heshima yake hata kama akija mwingine wa aina ipi.

Wakati Manchester United wanaitangaza Adidas kama mdhamini wa vifaa, kamwe hawakuondoa jina la mdhamini mkuu kwenye jezi zao.





Huenda mdhamini wa vifaa aliwashawishi Mbeya City kumpa nafasi yeye ili aonekane siku ya utambulisho, kama ni hivyo, bado walikosea sana.

Naamini bado wana muda wa kutafakari kurejea katika njia sahihi. Huu ni ushauri na wana haki ya kuuchukua au kuuacha, lakini vizuri wakaangalia katika njia sahihi inayoweza kuendeleza kuonyesha Mbeya City ni timu ya watu bila itikadi au ukabila. Pia vema kuwaheshimu wadhamini ambao wanajitolea katika soka, kumbukeni bado wana njia nyingine za kujitangaza, wanapowapa nafasi nyie, waonyesheni thamani yao kwa kuwathamini.



Powered by Blogger.