ABDULRAHMAN MUSA, SHUJAA WA RUVU SHOOTING, MKALI WA MABAO ALIYETIBIWA ZAIDI YA DAKIKA 15 KABLA YA KUFUNGA BAO LAKE LA 14
ABDULRAHMAN AKIWANIA MPIRA NA SIMON MSUVA, WOTE WAWILI WAMEFUNGA MABAO 14 KATIKA LIGI KUU BARA... |
Na Masau Bwire
MSHAMBULIAJI Abdulrahaman Musa wa Ruvu Shooting ndiye shujaa katika msimu huu wa Ligi ya VPL uliohitimishwa May 20, 2017.
Abdulrahaman
katika msimu huu wa Ligi amecheza dakika 2,700 katika michezo yote 30
iliyochezwa na kila timu pasipo kupumzika na kufanikiwa kufunga magoli
14 kati ya hayo, mawili yakiwa ya pinati.
Magoli
aliyofunga Abdulrahaman ni dhidi ya Simba (1), mzunguko wa kwanza,
Taifa, Yanga (1), mzunguko wa kwanza, Taifa, Ndanda Fc (1, penati),
mzunguko wa kwanza, Mabatini, Mbao (1), mzunguko wa kwanza, Mabatini,
JKT Ruvu (2), moja kila mchezo, nyumbani na ugenini, Majimaji (3),
mzunguko wa pili, Mabatini, Mbeya City (1), mzunguko wa pili, Sokoine,
Mbeya, African Lyon (1), mzunguko wa pili, Chamazi Complex, Mwadui (1,
penati), mzunguko wa pili, Mwadui Complex, Shinyanga na Stand United
(1), mzunguko wa pili, Kambarage Shinyanga.
Abdulrahaman
alizaliwa Januari Mosi, mwaka 1995, Hospital ya mkoa wa Mtwara, Ligula
akiwa mtoto wa tano kati ya watoto sita wa mzee Musa Abdulrahaman na
mama Somoe Salum.
Mwaka 2001 alianza masomo yake, darasa la kwanza na kuhitimu elimu ya msingi mwaka 2007.
Mwaka
2008 alianza masomo ya Sekondari katika shule ya Sekondari Mitengo,
Mikindani, Mtwara ambapo alihitimu kidato cha nne mwaka 2011.
Mwaka
2012, akichezea timu ya Korosho ya Mtwara iliyokuwa ikishiriki
mashindano ya mabingwa wa Mikoa kituo cha Mlandizi alionekana kuwa na
uwezo mkubwa wa kucheza mpira kiasi cha kumvutia kocha wa Ruvu Shooting,
kwa wakati Charles Boniface Mkwasa ambaye aliushawishi uongozi wa timu
kumsajili. Baada ya ligi hiyo kumalizika, Abdulrahaman alisajiliwa na
timu ya Ruvu Shooting akiwa mchezaji huru baada ya mkataba wake na timu
ya Korosho kumalizika.
Akiwa
na timu ya Ruvu Shooting alionesha uwezo na umahili mkubwa katika
kucheza mpira ambapo, mwaka 2013 aliajiriwa na Jeshi la Kujenga Taifa
(JKT) na kufanya kazi (Askari) Kikosi cha Jeshi 832, Ruvu JKT .
Msimu
wa ligi ya VPL, 2014/15 timu ya Ruvu Shooting ilishuka daraja,
Abdulrahaman akaenda kuichezea kwa mkopo timu ya JKT Ruvu msimu wa
2015/16.
Akiwa
huko, aliendelea kung'ara ambapo msimu wa ligi 2015/16 alichaguliwa
kuwa mchezaji bora wa VPL, mwezi May baada ya kuisaidia timu yake
kushinda michezo miwili mfululizo, dhidi ya Ndanda alifunga magoli
mawili na Simba uwanja wa Taifa pia akafunga magoli mawili.
Msimu
huu wa ligi VPL, Ruvu Shooting ilimrejesha kikosini ambapo aliendelea
kutema cheche na kuonesha kiwango kikubwa mno cha kucheza mpira ambapo
mwezi April alichaguliwa kuwa mchezaji bora wa VPL mwezi April na
kukabidhiwa kitita cha Tsh 1,000,000 kutoka kwa mdhamini, Kampuni ya
simu za mkononi Vodacom.
Abdulrahaman
mbali ya uwezo mkubwa wa kucheza mpira, ni mwenye nidhamu ya hali ya
juu nje na ndani ya uwanja. Hili linadhihirishwa na kumaliza musimu
mzima wa ligi, mechi 30 alizocheza kwa jumla ya dakika 2,700 alikanywa
mara moja tu kwa kadi ya njano na mwamuzi Mbaraka Rashid katika mchezo
dhidi ya Majimaji uliofanyika Mabatini.
Abdulrahaman ni mchezaji mwenye nguvu, maarifa na akili katika mpira, ni mvumilivu, hachoki wala hakati tamaa awapo uwanja.
Katika
mchezo wa mwisho wa VPL, 2016/17 uliofanyika May 20, dhidi ya Stand
United, Kambarage, kijana huyo alishangaza wengi kwa mengi katika
uchezaji wake wa mpira namna anavyo haha uwanja mzima japo yeye hucheza
pembeni (winger) kushpto na kulia.
Dakika
ya 60 ya mchezo, Abdulrahaman aliumia vibaya, alipasuka kichwa baada ya
kupigwa kichwa na beki wa Stand, akatokwa na damu nyingi katika jeraha
hilo la upande wa kushoto wa kichwa chake, juu kidogo ya sikio, jeraha
lililoshonwa nyuzi tatu na daktari wa timu Genoveva Kampala.
Haikuwa
rahisi kwa hali ya jeraha hilo, namna damu zilivyokuwa zikimtoka,
kurudi tena uwanjani na kucheza kwa kasi ile ile na hatimaye kupachika
goli lililomfanya awe mfungaji bora. Tulishuhudia mchezaji mmoja mahili
aligongana na mchezaji mwenzake uwanja wa Taifa akaumia kidogo kichwani,
alizirai! Hapo unaiona tofauti ya dona na viazi dume!
Matibabu ya kulishona jeraha hilo yalimchukuwa Daktari Kampala dakika 17, toka dakika ya 60 ya mchezo hadi dakika 77.
Pamoja
na maumivu, Abdulrahaman aliomba nafasi yake isifanyiwe marekebisho
akidai atashonwa jeraha, ataingia kucheza hatakama imebaki dakika moja
ili atafute goli litakalompa kiatu cha dhahabu!
Ndoto
ya mchezaji huyo Kinda ilitimia kwani, baada ya kuingia dakika ya 77,
alicheza kama hajaumia popote, juhudi zake zikazaa matunda kwa kufunga
goli safi dakika ya 89.
Abdulrahaman Musa ameoa, ana mke, Swaiba Abdallah Kaisi na mtoto mmoja, Wahda Abdulrahaman.
Mwandishi
wa makala haya, ni msemaji wa klabu ya Ruvu Shooting, pia ni mwalimu wa
Shule ya Msingi Makumbusho ya jijini Dar es Salaam.