|
Mafundi wa TANESCO wakiwa kwenye ukaguzi katika eneo la Chalinze (Sub-station) ambapo laini ya umeme unaoelekea katika mtambo wa Ruvu Juu inapoanzia. |
|
Mtaalam wa Kitengo cha Umeme Mkubwa wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Mhandisi Emmanuel Haule (kushoto) akikagua mitambo mipya inayotarajiwa kupokea umeme na kutembeza pampu mpya. |
|
Mafundi
wakiwa kazini kuunganisha nyaya toka katika laini ya umeme inayotoka
Chalinze (Sub-station) na kuiingiza katika laini ya Ruvu Juu ili iweze
kuongeza nguvu ya umeme kwa ajili ya kuzalisha maji zaidi. |
|
Hii ni Transfoma mpya iliyopo katika eneo la Mtambo wa Ruvu Juu ambalo kwa sasa linafanya kazi vizuri ya kutoa umeme kwa ajili ya mitambo. |
|
Mtambo mpya wa kusukuma maji wa Ruvu Juu kama unavyoonekana, mtambo huu unafanya kazi vizuri ya kusukuma maji. |
|
Hii ni sehemu ya mtambo wa kuwashia na kuongoza mitambo inayofanya kazi ya kusukuma maji eneo la Ruvu Juu kama unavyoonekana. |
|
Hili
ni eneo la mtambo wa maji wa Ruvu Juu ambapo maji husafishwa na kisha
kupelekwa katika mtambo mwingine kwa usafishaji zaidi na kisha
kusafirishwa kwa wananchi. |
|
Hili ni jengo la Utawala la Ruvu Juu ambapo shughuli za masuala ya maji zinafanywa na watendaji wake. |
|
Hili
ni eneo la mtambo wa maji wa Ruvu Juu ambapo maji yaliyosafishwa toka
mitamboni hupitia ikiwa ni hatua ya mwisho tayari kusafirishwa kwenda
kwa wananchi. |
|
Hili
ni bomba kubwa la maji safi la Ruvu Juu ambapo maji yaliyosafishwa toka
mitamboni hupitia na kupelekwa sehemu ya kuyasafirisha kwenda kwa
wananchi. |
|
Hili
ni eneo la mtambo wa maji wa katika eneo la IN TAKE lililopo katika Mto
Ruvu na ndiyo sehemu maji hunyonywa na mitambo na kuyapeleka eneo la
Ruvu Juu kwa ajili ya kusafishwa. |
|
Hii ni sehemu ya mtambo wa kuwashia na kuongoza mitambo inayofanya kazi ya kusukuma maji eneo la IN TAKE lililopo Mto Ruvu. |
|
Hii
ni mitambo ya kusukuma maji iliyopo katika eneo la IN TAKE katika eneo
la Mto Ruvu na ndiyo sehemu inayofanya kazi ya kukusanya na kusukuma
maji kuelekea Ruvu Juu. |
|
Hili
ni jengo la IN TAKE ambapo ndani ndipo iliposimikwa mitambo inayotumika
kusukuma maji kuelekea eneo la Ruvu Juu kwa ajili ya kusafishwa na
kusambazwa kwa wananchi. |
|
Hili ni Transfoma kubwa lenye uwezo wa 45/55 MVA na ndiyo linalotoa umeme kupeleka eneo la Ruvu Juu kwa ajili ya kusukuma maji. |
|
Nguzo
unazoziona upande wa kulia kwa mbali ndiyo laini ya umeme ilipopita
kutoka katika Transfoma inayotoa nguvu ya umeme ya 45/55 MVA, hivyo
nyaya za umeme zimepitishwa chini kuelekea katika nguzo hizo
zinazoonekana ambazo nazo husafirisha umeme huo kwenda Ruvu Juu. |
(PICHA/HABARI NA MWANDISHI WETU)
KAZI ya ujenzi wa laini mpya ya umeme
wenye nguvu ya 33KV kutoka Chalinze (Sub-station) kwenda Mlandizi yenye urefu
wa kilomita 45 kwa lengo la kuongeza umeme ili kukidhi mahitaji ya upanuzi wa
mtambo uliofanyika na kuweza kusukuma ujazo wa lita za maji milioni 196 kwa
siku sasa umekamilika na majaribio ya matumizi ya laini hiyo yameanza kwa
matarajio ya kukamilisha kazi hiyo ndani ya siku mbili.
Taarifa ya Mamlaka ya Maji Safi na Maji
Taka Dar es Salaam (DAWASA) ilifafanua kwamba, DAWASA kupitia Mkandarasi wake
M/s WABAG kutoka nchini India kwa kushirikiana na Mkandarasi Msaidizi, Kampuni
ya M/s Mollel Electrical Contractors ya hapa nchini kwa sasa wamemaliza
kazi zote za ujenzi wa laini kutoka Chalinze mpaka eneo la kuingizia umeme
ndani ya Mtambo wa Maji wa Ruvu Juu uliopo Mlandizi tayari kwa majaribio ya
awali ya kiusalama na kuwasha pampu.
Mtambo huo wa maji wa Ruvu Juu utakua
ukipokea umeme wa kutosha kutoka katika transfoma kubwa iliyopo kituo kidogo
cha umeme Chalinze (Sub-station) yenye uwezo wa 45/55 MVA ambapo itawezesha
pampu zote mpya zilizofungwa kuwashwa.
Hapo awali mtambo huo ulikuwa na
uwezo wa kuzalisha lita milioni 82 kwa siku na mara baada ya majaribio haya na
kuongeza umeme ndani ya siku mbili uzalishaji wake utaongezeka kufikia lita
milioni 196 kwa siku.
Taarifa ya DAWASA inabainisha kuwa, ili
lita hizo milioni 196 za maji ziweze kusukumwa na mtambo huo wa Ruvu Juu,
mtambo unahitaji 16MVA za umeme ili kusukuma maji safi yanayozalishwa baada ya
upanuzi kwa asilimia100.
Aidha, Mkandarasi kwa sasa amekamilisha
kazi ya kujenga laini hiyo mpya toka sub-station ya Chalinze ikiwa ni pamoja na
kazi zote zilizotakiwa kufanyika ndani ya kituo hicho kidogo cha umeme cha
Chalinze. Hizo ni pamoja na kazi mbalimbali zilizotakiwa kufanyika ili kuweza
kuupokea umeme huo kutoka kwenye transfoma hiyo.
Aidha, maeneo nufaika ya mtambo wa maji
wa Ruvu Juu ni Mkoa wa Dar es Salaam, mkoa wa Pwani, maeneo ya mji wa Mlandizi,
Kibaha na baadhi ya Vitongoji vyake.
DAWASA inaendelea kulishukuru Shirika
la Umeme Tanzania (TANESCO) kwa ushirikiano na ushauri wa kitaalam kuhusiana na
masuala ya umeme ambao imekua ikiutoa mara kwa mara ili kuhakikisha kuwa maji
ya kutosha yanapatikana katika jiji la Dar es Salaam na maeneo yote
yanayohudumiwa na DAWASA.
Mikataba ya upanuzi wa mtambo na ujenzi
wa mabomba mapya kutoka Ruvu Juu mpaka Kimara pamoja na ujenzi wa tanki kubwa
lenye ujazo wa lita million 10 ilisainiwa mwaka 2014 na Serikali kupitia Wizara
ya Maji na Umwagiliaji ilipata fedha hizo kwa mkopo wa masharti nafuu toka
Benki ya Exim ya India.