Judith Ferdinand, Mwanza
Watoto wanaoishi katika mazingira magumu jijini Mwanza wameiomba
serikali,wadau,wafadhili na jamii kwa ujumla, kuwapa
kipaumbele,kuwalinda,kuwasikiliza na kuwasaidia.
Ikumbukwe kuwa yapo madhara makubwa, tukiacha jamii iwe na watoto
wanaoishi mtaani na endapo hali hii ikiendelea kukua taifa la baadaye na
ulimwengu vitakua hatarini.
Hayo yalisemwa jana na watoto wanaoishi katika mazingira magumu katika
maadhimisho ya siku ya Watoto wanaoishi mtaani duniani,yenye kauli mbiu
"Mtujali watoto tunaoishi mtaani,huu ni muda wetu" yaliyofanyika
kwenye uwanja wa Furahisha mkoani Mwanza, nakuandaliwa na Shirika la
Railway Children Afrika nchini Tanzania na kushirikiana na wadau
mbalimbali.
Mmoja wa watoto walioashiriki katika maadhimisho hayo Vumilia Mlasa
alisema,wao ni watoto kama wengine,wanaitaji kusikilizwa,kupendwa na
kupatiwa mahitaji,hivyo wanaiomba serikali,jamii na wafadhili kuwasaidia
ili kufikia malengo yao.
"Sisi watoto tuliopo katika mazingira magumu, tunaomba wadau kwa
ujumla,muendelee kutusaidia,tuchukulieni kama ndugu na
rafiki,tupendeni,mtuthamini,tulindeni,mtujali,tuleeni vema pamoja na kutupatia elimu," alisema Mlasa.
Kwa upande wake Emmanuel John alisema, wanaimani wadau wakiwajibika
ipasavyo,itawasaidia siku za usoni kuwa watu wema sambamba na kuwaomba
wazazi na walezi kuhakikisha familia ni mahali salama pa kuishi,jambo
litakalosaidia kupunguza ongezeko la watoto wa mitaani.
Naye Afisa Ustawi wa Jamii mkoa wa Mwanza Wambura Kizito ambaye ndiye
mgeni rasmi katika maadhimisho hayo, aliwaomba wadau kuendelea
kushirikiana na serikali kusaidia watoto hao sambamba na wazazi na jamii
kila mmoja kuwajibika kwa nafasi yake,ili kumaliza tatizo la watoto wa
mtaani na kuwa na taifa bora baadae.
Hata hivyo Meneja Mradi wa Railway Children Africa Aneth Isaya alisema,
mpaka sasa shirika hilo linahudumia zaidi ya watoto 200,licha ya
kukumbana na changamoto kutoka kwa watoto hao,ambao wamekuwa wakitoa
taarifa za uongo za mahali walipotoka na jina,ikiwa ni jitihada za
kuwarudisha kwao.
Isaya alisema, kumekuwa na ongezeko la watoto wa mitaani ukilinganisha
na miaka iliyopita,ambapo chanzo ikiwa ni familia wazazi kukosa upendo,
kutowasikiliza wanachohitaji pamoja na hali ngumu ya maisha.
Pia aliiomba,serikali iwasaidie kuwa na mfumo rahisi utakaotumika wakati
wa kuwarudisha nyumbani kwao pamoja na kujitoa na kuunga mkono kundi
hilo moja kwa moja kama ilivyo kwa watoto wengine.