JUMIA TRAVEL: JAMII IKIUNGE MKONO KITUO CHA YATIMA CHA MALAIKA.
Meneja Uhusiano wa
Umma wa Jumia Travel nchini Tanzania, Geofrey Kijanga, akizungumza na
waandishi wa habari Dar es Salaam leo wakati wafanyakazi wa kampuni hiyo walipokitembelea Kituo cha kulelea watoto wanaoshi katika mazingira magumu cha Malaika Kids Tanzania na kutoa msaada wa vyakula na vitu mbalimbali kwa ajili ya Sikukuu ya Pasaka. Kituo hicho kipo Kinondoni jijini Dar es Salaam.
Mwanzilishi na
Ofisa Mtendaji Mkuu wa kituo cha Malaika Kids Reception, Najma Manji
akizungumza na wanahabari kuhusu kituo hicho.
Meneja Uhusiano wa
Umma wa Jumia Travel nchini Tanzania, Geofrey Kijanga (kulia),
akimkabidhi Ofisa Mtendaji Mkuu wa Kituo hicho msaada huo.
Meneja Uhusiano wa
Umma wa Jumia Travel nchini Tanzania, Geofrey Kijanga (kulia)
akimkabidhi katoni ya sabuni Leila Mustafa anayelelewa katika kituo
hicho
Ofisa kutoka Jumia Travel, Patricia Muthama, akimkabidhi msaada huo, Amina Rodvick anayelelewa kwenye kituo hicho.
Ofisa wa Jumia Travel, Mustafa Ali (kulia), akimkabidhi
msaada huo mtoto, Najma Mohamed
Muonekano wa vitanda vinavyotumiwa na watoto wa kituo hicho.
Kituo hicho kinavyoonekana kwa nje.
Na Dotto Mwaibale
JAMII imetakiwa kuunga mkono jitihada za
kituo cha kulelea watoto wanaoshi katika mazingira magumu cha Malaika
Kids Tanzania kinachopokea watoto, kuwalea, kuwasomesha na kuwatafutia
kazi ili kuweza kujitegemea.
Hayo yamesemwa na Meneja Uhusiano wa
Umma wa Jumia Travel nchini Tanzania, Geofrey Kijanga Dar es Salaam leo
wakati wafanyakazi wa kampuni hiyo walipokitembelea na kutoa msaada wa
vyakula na vitu mbalimbali kwa ajili ya sikukuu ya Pasaka.
“Kwanza kabisa ningependa kuchukua fursa
hii kuupongeza uongozi wa kituo cha Malaika Kids Reception kwa jitihada
wanazozifanya. Kuanzisha kituo cha kuwapa hifadhi watoto ambao wanakosa
malezi aidha kutokuwa na wazazi, ndugu au kutelekezwa mitaani kuna
changamoto nyingi. Lakini changamoto hizo zinawezekana endapo tu jamii
itaungana kwa pamoja kwa kutoa msaada wa hali na mali, uwe mdogo au
mkubwa ili kuvipa uwezo vituo hivi,” alisema Kijanga.
“Kuna usemi unaosema mcheza kwao
hutunzwa, nasi kama Jumia Travel Tanzania tukiwa tunafanyia shughuli
zetu eneo hili tumeonelea ni vema kwa kuanza kusaidia jamii
inayotuzunguka kabla ya kwenda mbali zaidi. Tunaunga mkono juhudi
zinazofanywa na kituo hiki kwani hawa watoto wanaolelewa hapa nao
wanatamani wangekuwa wanaishi na familia zao. Kwa kufanya hivi tunaamini
kuwa tutakuwa tunaikumbusha jamii ya watanzania kuwa tatizo la watoto
yatima au wa mitaani lipo na linahitaji nguvu za ziada katika kupamba
nalo,” aliongezea Meneja huyo wa Uhusiano wa Umma kampuni inayojihusisha
na huduma za hoteli kwa njia ya mtandao.
“Ningependa kutoa wito kwa kampuni
nyingine, serikali, watu binafsi na jamii kwa ujumla kukitupia macho
kituo hiki na kuunga mkono jitihada wanazozifanya. Nilifanya mazungumzo
na Mkuu wa kituo hiki na amenieleza kuwa mbali na kuwalea watoto lakini
pia wanawasomesha pamoja na kuwatafutia ajira ili waweze kuanza maisha
yao ya kujitegemea. Hivyo ili kukipunguzia mzigo kituo hiki, jamii
inaweza kusaidia kusomesha baadhi ya watoto au kuwatafutia kazi wale
wanaomaliza masomo yao,” alisema Kijanga.
Mwanzilishi na Ofisa Mtendaji Mkuu wa
kituo cha Malaika Kids Reception, Najma Manji amesema kuwa inatia moyo
kuona jamii inayozunguka inatambua uwepo wao na kujitokeza kuwasaidia.
“Kwanza kabisa ni jambo la kumshukuru
Mungu kuona kwamba jamii inayotuzunguka inatambua jitihada tunazozifanya
katika kuwalea watoto wanaoishi katika mazingira magumu. Hatua ya
kuanzisha kituo hiki sikuifanya kana kwamba ninao uwezo mkubwa, la
hasha, bali ni kwa kuguswa tu na magumu wanayoyapitia watoto hawa
wanaokosa msaada. Na huwa najaribu kuvuta picha kama endapo wangekuwa ni
watoto wangu,” alisema Manji.
Akielezea kwa ufupi shughuli
wanazozifanya kituoni hapo pamoja na changamoto wanazokumbana nazo
mwanzilishi wa kituo hiko alisema kuwa, “Mpaka hivi sasa tunao watoto
takribani 80, sina idadi kamili ya wanawake ni wangapi na wanaume ni
wangapi lakini wanaume ni wengi kidogo kuliko wanawake. Tunawapokea
watoto kuanzia miako 0 mpaka 7 kutoka ustawi wa jamii, hatupendelei
watoto wanaozidi umri huo kwani inakuwa ni vigumu kuwabadili tabia zao.”
“Mbali na malezi lakini pia
tunawasomesha pamoja na kuwatafutia kazi ili waweze kujitegemea. Kwa
mfano, hivi sasa tunao wawili ambao wamekwisha maliza masomo yao katika
masuala ya hoteli lakini bado hawajapata kazi. Na tayari kuna wengine
ambao walishalelewa hapa na kusomeshwa wapo makazini wakijetegemea na
maisha yao. Ningependa kutoa wito kwa watanzania wenzangu kuja
kutusaidia kwa chochote walichonacho iwe ni vyakula, nguo, vifaa vya
shule, kusaidia kulipa ada na hata kuwatafutia au kuwapa kazi wale
wanaohitimu masomo yao ili nao waweze kujitegemea na kuendelea na maisha
yao,” alisema Manji.
Msaada wa vyakula uliotolewa na
wafanyakazi wa kampuni hiyo walipotembelea kwenye kituo hiko ni pamoja
na unga, mchele, maharage, mafuta ya kupikia, sukari, chumvi, sabuni na
mengineyo. Dhumuni kubwa la kufanya hivyo ni kuwafanya watoto hao nao
kufurahia sikukuu ya Pasaka itakayosherehekewa siku ya Jumapili na
Jumatatu duniani kote.