SERIKALI KUWEKEZA KWENYE VIFAA TIBA VITOKANAVYO NA PAMBA.
Na Daudi
Manongi-MAELEZO, DODOMA.
Serikali
kupitia Mfuko wa Bima ya Afya (NHIF) unakamilisha taratibu za uwekeza kwenye
vifaa tiba vitokanavyo na pamba na bidhaa za maji ya dripu(Infusion Fluids).
Hayo yamesemwa
leo na Waziri wa Viwanda,Biashara na Uwekezaji Mhe.Charles Mwijage wakati
akijibu hoja mbalimbali za wabunge mjini Dodoma.
“Gharama za
miradi hii inakadiriwa kufikia dola za kimarekani milioni 36.5 na kutoa ajira za
moja kwa moja 1600 na zisizo za moja kwa moja 5000”, Alisema Mhe.Mwijage.
Amesema mradi
huu unakadiriwa kutumia pamba tani elfu 50 kwa mwaka na Serikali ya Mkoa wa
Simiyu inaendelea na jitihada za kutenga maeneo ya uwekezaji kwa kuwalenga
wajasiriamali wadogo,wa kati mpaka wakubwa bila kujali kama ni wa kutoka ndani
au nje ya nchi.
Aidha amesema
kuwa azma ya Serikali ya ujenzi wa uchumi wa viwanda imeainishwa vyema katika
mpango wa pili wa Maendeleo wa miaka mitano wa mwaka 2016/17-2020/21 wenye
dhima ya kujenga uchumi wa viwanda ili kuleta mageuzi ya kiuchumi na maendeleo
ya watu.
Pamoja na hayo
ameainisha kuwa ili kufikia azma hiyo ushiriki wa mchango wa mtu mmoja
mmoja,makundi ya watu,taasisi za umma na taasisi binafsi unahitajika.