WAZIRI WA AFYA ATAJA VIPIMO NA DAWA ZA MALARIA ZINAZOTAKIWA KUTOLEWA BURE KWA WANANCHI
Serikali ya Tanzania imepiga marufuku
vituo vya Umma kuwalipisha wananchi wanaokwenda kupima maambukizi ya
ugonjwa wa Malaria kwa kipimo cha MRDT na utoaji wa dawa za mseto (ALUU)
zinazotumika kutibu ugonjwa huo kuanzia sasa.
Akizungumza na waandishi wa habari
wakati wa kilele cha maadhimisho ya siku ya Malaria duniani mjini
Dodoma, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Bi.
Ummy Mwalimu amesema vipimo hivyo ni bure na pia mgonjwa asilipishwe
fedha kwa dawa za mseto.
“Napenda kusisitiza vituo vya umma
vinavyotumia vipimo vya MRDT kwa wagonjwa wa malaria, vipimo hivyo ni
bure na pia mgonjwa asilipishwe fedha kwa dawa za mseto ama yule
anayelazwa kuchomwa sindano ya ugonjwa huo….Waganga wakuu wa mikoa na
wilaya, hakikisheni kuanzia sasa mnafuatilia wahudumu wote na
watakaokiuka agizo hili watachukuliwa hatua za kisheria mara moja”.
Alisema Bi. Ummy
Aidha, Bi. Ummy amewataka wananchi
kushirikiana na serikali kuwafichua wahudumu wa Afya ambao watawalipisha
fedha pindi watakapo kuwa wanapima huduma ya Malaria kupitia kipimo cha
MRDT ama watakapohitajika kupewa dawa ya mseto (ALUU), pia amezionya
maabara binafsi ambazo zimekuwa zikifanya kazi zake kwa kuangalia zaidi
fedha badala ya maisha ya mtu kama kuwaambia wana maambukizi ya malaria
wakati hawana.
Pamoja na hayo, amesema takwimu kutoka
katika vituo vinavyotolea huduma za afya zinaonyesha takribani watu
milioni 12 wanaugua ugonjwa huo kwa mwaka ambapo katika tafiti hizo mkoa
wa Kagera, Geita na Kigoma ziliweza kuonekana na viwango vikubwa vya
maambukizo kwa mwaka 2015 na 2016 huku wajawazito na watoto chini ya
miaka mitano kuonekana kuathiriwa zaidi.