RAIS MAGUFULI ATOA MSAMAHA KWA WAFUNGWA MAADHIMISHO YA MIAKA 53 YA MUUNGANO WA TANZANIA
Katika
kuadhimisha Miaka 53 ya Muungano wa Tanzania tarehe 26 Aprili, 2017
Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutumia madaraka
aliyopewa chini ya Ibara ya 45(1)(d) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania ametoa msamaha kwa wafungwa wafuatao:-
Wafungwa
wote ambao baada ya punguzo la kawaida la moja ya tatu (1/3)
linalotolewa chini ya Kifungu 49(1) cha Sheria ya Magereza Sura ya 58,
wawe wametumikia nusu (½) ya vifungo vyao vilivyobaki, isipokuwa
wafungwa walioorodheshwa katika Ibara ya 2(i – xxi).
Wafungwa
wagonjwa wenye magonjwa kama UKIMWI, Kifua kikuu (TB) na Saratani
(Cancer) ambao wako kwenye “terminal stage”. Wafungwa hawa wathibitishwe
na Jopo la Waganga chini ya Uenyekiti wa Mganga Mkuu wa Mkoa/Mganga
Mkuu wa Wilaya.
Wafungwa
wazee wenye umri wa miaka sabini (70) au zaidi. Umri huo uthibitishwe
na Jopo la Waganga chini ya Uenyekiti wa Mganga Mkuu wa Mkoa/Mganga Mkuu
wa Wilaya.
Wafungwa wa kike walioingia na mimba gerezani, pamoja na wale walioingia na watoto wanaonyonya na wasionyonya.
Wafungwa
wenye ulemavu wa mwili na akili (Physical disability and mental
disability). Ulemavu huo uthibitishwe na Jopo la Waganga chini ya
Uenyekiti wa Mganga Mkuu wa Mkoa/Mganga Mkuu wa Wilaya.
Aidha, Msamaha huu wa Mheshimiwa Rais hautawahusu wafungwa wafuatao:-
Wafungwa waliohukumiwa adhabu ya kunyongwa.
Wafungwa waliohukumiwa adhabu ya kunyongwa na adhabu hiyo kubadilishwa kuwa kifungo cha maisha au kifungo gerezani.
Wafungwa waliohukumiwa kifungo cha maisha gerezani.
Wafungwa
wanaotumikia kifungo kwa makosa ya kujihusisha na usafirishaji na
matumizi ya madawa ya kulevya kama vile cocaine, heroin, bhangik.
Wafungwa wanaotumikia kifungo kwa makosa ya kujihusisha na uombaji na upokeaji au utoaji rushwa.
Wafungwa
wanaotumikia kifungo kwa makosa ya unyang’anyi na unyang’anyi wa
kutumia silaha au kujaribu kutenda makosa hayo (robbery with violence,
armed robbery and attempt robbery).
Wafungwa
wanaotumikia kifungo kwa makosa ya kupatikana na silaha, risasi au
milipuko isivyo halali (fire arms, ammunitions and explosives).
Wafungwa wanaotumikia kifungo kwa makosa ya shambulio la aibu, kunajisi, kubaka na kulawiti au kujaribu kutenda makosa hayo.
Wafungwa
waliopatikana na hatia na kuhukumiwa kifungo kwa kosa la kuwapa mimba
wanafunzi wa Shule za Msingi na Shule za Sekondari na ambao walitenda
kosa hilo wakiwa na umri wa miaka kumi na nane (18) na kuendelea.
Wafungwa
wanaotumikia kifungo kwa makosa ya wizi wa magari na pikipiki,
uharibifu wa miundombinu au kujaribu kutenda makosa hayo.
Wafungwa
wanaotumikia kifungo chini ya Sheria ya Bodi ya Parole (Act. No.
25/1994) na Sheria ya Huduma kwa Jamii (Act. No. 6/2002).
Wafungwa waliopatikana na hatia na kuhukumiwa kifungo kwa makosa ya kutumia vibaya madaraka yao.
Wafungwa
waliowahi kupunguziwa kifungo na Msamaha wa Mhe. Rais na bado wangali
wanaendelea kutumikia sehemu ya kifungo kilichobaki.
Wafungwa waliopatikana na hatia na kuhukumiwa kwa kosa la kuzuia watoto kupata masomo.
Wafungwa
waliopatikana na hatia na kuhukumiwa kwa kosa la utekaji wa watoto,
kupoka na kufanya biashara ya binadamu (Human Trafficking).
Wafungwa waliopatikana na hatia na kuhukumiwa kwa kosa la kukutwa na viungo vya binadamu.
Wafungwa wanaotumikia vifungo kwa makosa ya kujihusisha kwa namna yoyote ile na nyara za Serikali na ujangili (poachers).
Wafungwa wanaotumikia vifungo kwa makosa ya wizi/ubadhirifu wa fedha za Serikali.
Wafungwa wanaotumikia vifungo kwa makosa ya kutoroka au kujaribu kutoroka chini ya ulinzi halali.
Wafungwa walioingia gerezani baada ya tarehe 16/03/2017.
Wafungwa warejeaji wa makosa/wafungwa waliowahi kufungwa gerezani (Recidivists).
Wafungwa
2,219 watafaidika na msamaha huu na wataachiliwa huru. Ni mategemeo ya
Serikali kwamba watarejea tena katika jamii kushirikiana na wenzao
katika ujenzi wa Taifa na kwamba watajiepusha kutenda makosa ili
wasirejee tena gerezani.
Meja Jenerali Projest Rwegasira
KATIBU MKUU
WIZARA YA MAMBO YA NDANI YA NCHI