RAIS MAGUFULI: YEYOTE ATAKAYEJARIBU KUVUNJA MUUNGANO ATAVUNJIKA YEYE
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe
Magufuli, leo tarehe 26 April 2017, ameongoza maelfu ya Watanzania
katika sherehe za miaka 53 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar
zilizofanyika katika Uwanja wa Jamhuri Mjini Dodoma.
Akizungumza mara baada ya kukagua gwaride la vikosi vya ulinzi na
Usalama lililoandaliwa kwa heshma yake, Rais Magufuli amewahakikishia
watanzania kuwa yeye na Rais wa Zanzibara Dkt. Ali Mohamed Shein
wataendelea kuulinda Muungano kwa nguvu zao zote na kwamba atakayejaribu
kuuvunja atavunjika yeye.
''Muungano ndio silaha yetu. Ni nguvu yetu. Mimi na mwenzangu Dkt. Shein
tutaulinda Muungano kwa nguvu zote. Yeyote atakayejaribu kuuvunja
atavunjika yeye'' amesema Rais Magufuli.
Aidha Dkt. Magufuli amewataka watanzania kuendelea kudumisha amani
iliyopo nchini kwani amani ndio chachu ya maendeleo yanayopatikana
nchini.
Rais Magufuli amesema Tanzania imeweza kufikisha miaka 53 ya Muungano wa
Tanganyika na Zanzibar kwa sababu ya amani iliyopo nchini iliyowezesha
kupatikana mafanikio makubwa ikiwa ni pamoja na kuunganisha mataifa yetu
mawili na kuuunda taifa moja lenye nguvu.
Aidha amesema Muungano wa Tanganyika na Zanzibar umewezesha kupatikana
mafanikio makubwa katika nyanja za kiuchumi, kisiasa na kijamii.
Mhe. Rais ametaja mafanikio mengine yaliyopatikana kutokana na Muungano
ni kukua kwa uchumi na kukabiliana na matatizo ya umasikini na ukosefu
wa ajira,kuimarisha miundombinu ya usafiri wa anga, majini,reli na nchi
kavu.
Aidha Muungano umeimarisha na kuboresha upatikanaji wa huduma za jamii
ikiwa ni pamoja na kuongezeka kwa idadi ya shule na hospitali pamoja na
kukua kwa demokrasia nchini.
Kwa mara ya kwanaza katika historia ya Muungano wa Tanganyika na
Zanzibar Maadhimisho ya Sherehe za Muungano zinafanyika mkoani Dodoma
makao makuu ya Serikali ikiwa ni ishara tosha kuwa Serikali ya awamu ya
tano inayoongozwa na chama cha Mapinduzi imedhamiria kwa dhati
kuhakikisha makao makuuu ya Serikali yanakuwa Dodoma.
''Niwahahakikishie wana Dodoma na Watanzania kwa ujumla kwamba Serikali
sasa tumefika Dodoma na hatutarudi tena, na kama tulivyoahidi mwaka
2020 Serikali yote itakuwa imehamia hapa'' amesema Rais magufuli.
Sherehe za miaka 53 ya Muungano zimehudhuriwa na viongozi mbalimbali
ikiwa ni pamoja na wajane wa viongozi waasisi wa Muungano mke wa hayati
Mwalimu Julius Nyere Mama Maria Nyerere na hayati Abeid Aman Karume,
Mama Shadya Karume,Makamu wa Rais Mama Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu
Kassim Majaliwa, na viongozi wa chama na serikali.
Kauli mbiu ya Sherehe za Muungano mwaka huu ni ''Miaka 53 ya
muungano,Tuuulinde na kuuimarisha, Tupige vita Dawa za Kulevya na
Kufanya Kazi kwa Bidii''
Jaffar Haniu
Naibu Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dodoma
26 Aprili, 2017