Mke
wa Roma Mkatoliki, Nancy ambaye ni mama wa mtoto mmoja aitwae Ivan,
amedai yeye pamoja na ndugu zake wameshazunguka kila sehemu bila
mafanikio kumtafuta mume wake ambaye ametekwa usiku wa Jumatano hii
akiwa studio za Tongwe Record Masaki jijini Dar es Salaam.
Akiongea
na waandishi wa habari jana jioni, Nancy alisema mara ya mwisho
kuzungumza na Roma ilikuwa juzi saa kumi na mbili jioni.
“Mimi
kama mke wa Roma mara ya mwisho niliwasiliana na mume wangu juzi saa
kumi na mbili jioni, akaniambia anaelekea Tongwe Records kwajili ya kazi
zake za kila siku. Baada ya hapo sikuwa nampata tena kwenye simu lakini
nikachukulia ni kawaida tu simu imezima, nimekuja kuamka saa 7
nikapokea simu kutoka kwa rafiki yake akaniambia uko na Roma nikamwambia
hapana alikuwa Tongwe, akaniambia kuna taarifa kwenye mitandanao na
mimi nikaingia nikakuta hizo taarifa kama walizopata watu wengine,” alisema Nancy na kuongeza:
“Baada
ya hapo nikaanza kutafuta watu wa kunisaidia, baadhi ya ndugu zangu
wameangaika vituo vyote vya polisi Roma hayupo, hadi sasa hivi sifahamu
yuko wapi, kwa ufupi sina ninachokijua wala ninachokifahamu. Jitihada
zangu za kutafuta kwenye vituo vyote vya polisi nimemaliza,”
Alisema mume wake huyo hakuwai kumpatia taarifa yoyote kama anatafutwa na polisi wala ana tatizo na mtu yeyote.
Pia
aliwaomba wadau mbalimbali pamoja na watanzania kwa ujumla kumuunga
mkono katika jitihada za kumtafuta mume wake ambaye mpaka sasa
hajulikani aliko.
Kamanda wa Polisi Kanda ya Dar es salaam Kamishna Simon Sirro amesema kuwa wamezipata taarifa hizo na wanazifanyia kazi.