Baadhi
ya Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wameibuka na
kupinga vikali gharama za matumizi ya Faru Fausta aliyepo katika Hifadhi
ya Ngorongoro, na kuongeza kuwa gharama hizo haziendani na uhalisia.
Mjadala
huo uliibuka mara baada ya Mbunge wa Babati Mjini, Pauline Gekul
(Chadema) kuuliza swali kwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne
Maghembe kuhusu mipango ya Serikali kwa Faru huyo.
Aidha,
akijibu swali hilo, Prof. Maghembe amesema kuwa Faru huyo anatumia
gharama kubwa za matunzo kwa sababu ni mzee na huwa anaugua mara kwa
mara.
“Hivi
sasa utafiti unafanyika kwa kumtumia Faru Fausta juu ya namna ya kuishi
na wanyama wa aina hiyo ili waweze kuishi maisha marefu, ni kweli
kufanya hivi ni gharama kubwa sana,”amesema Prof. Maghembe.
Gharama
za matunzo ya Faru Fausta kwa mwezi ni shilingi milioni 64, kiasi
ambacho kiliwashtua baadhi ya wabunge na kutaka muongozo zaidi wa kupata
taarifa za kina zaidi.
Hata
hivyo, kwa upande wake Mkuu wa Hifadhi ya Ngorongoro, Dkt. Fredy
Manongi amesema kuwa Faru Fausta ni Mzee na ana umri wa miaka 54, hivyo
alipokuwa porini alikuwa akishambuliwa na Fisi kitendo ambacho
kilimsababishia vidonda vingi.