MABWENI MAPYA CHUO KIKUU CHA DAR ES SALAAM KUCHUKUA WANAFUNZI 3,840
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Magufuli, amefanya
uzinduzi wa mabweni mapya ya wanafunzi wa chuo kikuu cha Dar es Salaam,
UDSM.
Rais Magufuli amesema kukamilika kwa mabweni hayo ya kisasa ndani ya
kipindi chini ya miezi minane ni ishara kuwa Tanzania inaweza. “Tukiamua
tunaweza tukafanya watu wakaona miujiza,” amesema.
Ameongeza kuwa wapo watu walibeza kuwa shilingi bilioni 10 zisingeweza
kukamilisha ujenzi huo na kwamba hawakumiani kuwa yasingeweza kujengwa
na Watanzania. Ameshauri kuwa mafanikio hayo yawe vifundisho kwa
viongozi wa serikali kutotoa tenda kwa wakandarasi wa nje zenye gharama
kubwa na kuwaacha wale wa ndani.
Kwa upande mwingine Rais amesema mabweni hayo yatalipiwa kwa shilingi
500 pekee, tofauti na 800 kwa mabweni mengine. Mabweni hayo yana uwezo
wa kuchukua wanafunzi 3,840.
Awali akizungumza kwenye uzinduzi huo, makamu mkuu wa chuo hicho,
Profesa Rwekaza Mukandala alissema mabweni hayo yana vitanda 1,920 vya
double decker, makabati 1,920, shelves za vitabu 1,920, meza, 1,920,
viti 3,840 magodoro 3,840.
“Tutahakikisha kuwa huduma zote muhimu kama vile cafeteria ya chakula,
maduka kwaajili ya mahitaji mbalimbali, zahanati, salon, kituo cha
polisi na nyinginezo vinapatikana hapa hapa,” alisema Profesa Mukandala.
Aliongeza kuwa ujenzi wa cafeteria umeshaanza na ikikamilika itakuwa na
uwezo wa kuchukua wanafunzi 500 kwa wakati mmoja. Amehakikisha kuwa chuo
kimejipanga kuhakikisha kuwa mabweni yanatunzwa na tayari wameshampata
msimamizi mkuu aliyepewa mafunzo maalum ya muda mfupi.
Prof Mukandala alimshukuru Rais Magufuli kwa namna alivyojitolea
kuhakikisha mabweni hayo yanakamilika kwa kufuatilia kwa ukaribu kila
hatua za ujenzi wake.
“Hili ni jambo kubwa sana na historia itaandikwa kwa herufi za dhahabu,” alisema.
Aliongeza kuwa wizara tatu zimehusika kwenye ujenzi wa mabweni hayo
ambazo ni Wizara ya Ulinzi na Jeshi la kujenga taifa, Wizara ya Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia.
Mawaziri wote wa wizara hizo Dr. Hussen Mwinyi, Profesa Makame Mbarawa
na Profesa Joyce Ndalichako walikuwepo.