MIILI YA ASKARI POLISI 8 WALIOUAWA PWANI YAAGWA...WAZIRI ATANGAZA KIAMA
WAZIRI
wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba amewatangazia kiama watu
wote waliohusika kuwaua askari polisi nane Kibiti wilayani Mkuranga
mkoani Pwani.
Akizungumza
wakati wa kuaga miili ya askari hao jijini Dar es Salaam jana asubuhi
Mwigulu alisema watu hao watakamatwa wote na kufikishwa kwenye mkono wa
sheria.
"Kitendo hiki cha mauaji kilichofanyika dhidi ya askari wetu hakivumiliki hata kidogo waliohusika tutawatafuta na kuwakamata"alisema Mwigulu.
Aliwaomba wananchi wa maeneo husika kutoa ushirikiano kwa jeshi la polisi ili kuwapata wahusika wa tukio hilo.
Katika
hatua nyingine Mwigulu ameitaka wizara husika kuhakikisha inatoa fidia
kwa ndugu wa askari hao na majeruhi badala ya kuchukua muda mrefu
kuitoa.
"Naomba fidia kwa askari hawa tuliowapoteza wakitumikia taifa itolewa haraka bila kucheleweshwa" aliongeza Mwigulu.
Mkuu
wa Jeshi la Polisi Nchini (IGP), Ernest Mangu alisema watuhumiwa wote
waliohusika kufanya mauaji hayo ni lazima watafikiwa na mkono wa dola.
Alisema
wananchi wa eneo hilo wanawafahamu wahusika hivyo amewaomba
washirikiane na polisi ili kuwapata vinginevyo nguvu itatumika.
Alisema linapotokea tukio kama hilo kuna baadhi
ya watu wamekuwa wakishabikia kupitia mitandao ya kijamii hivyo akatoa
onyo kuwa watakao bainika na wao watakamatwa kwa kutenda kosa.