KUFUNGIWA KWA MANARA, MASAU BWIRE AINGIWA HOFU, HII HAPA KAULI YAKE



Baada ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kupitia kamati yake ya maadili kumfungia Msemaji wa Simba, Haji Manara, msemaji wa Ruvu Shooting, Masau Bwire ameibuka na kusema kuwa ameingia na hofu kutokana na tukio hilo.

Kamati ya Maadili ya TFF, imemfungia Manara kutojihusisha na masuala ya soka kwa kipindi cha miezi 12, na faini ya shilingi milioni tisa baada ya kukutwa na makosa matatu ya kinidhamu dhidi ya TFF ikiwa ni kitendo chake cha kuituhumu kutokana na utendaji wake.

Aidha, ukiachana na Manara ambaye amefungiwa wikiendi iliyopita pia, TFF kupitia kamati yake hiyohiyo ya maadili ilimfungia msemaji wa Yanga, Jerry Muro kutojihusisha na masuala ya soka kwa mwaka mmoja Julai mwaka jana.
Masau amesema kuwa amesikitishwa na hatua aliyochukuliwa ya Manara kufungiwa mwaka mmoja na kudai kuwa kitendo hicho kinatoa hofu kwa wasemaji wengine.

“Nimesikitishwa na hukumu ya Haji kama binadamu mwenye roho ya huruma mkiwa mnafanya kazi pamoja kisha mwenzio akaondolewa haileti picha nzuri, nilihitaji kupata chalenji kutoka kwake, kwani ukiwa na mwenzako wa upande wa pili mkiwa mnajibizana ndipo unapopata akili na kujifunza kunakosababisha kupata ubunifu zaidi.

“TFF wanatakiwa waangalie siyo kila kosa wanakimbilia kutoa adhabu kubwa na kumfungia mtu, wanatakiwa wawape onyo kwanza, hivyo hali hii inaogopesha watu wengine kuzungumza,” alisema Bwire.
Powered by Blogger.