WAZIRI NAPE NNAUYE ATANGAZA RASMI KUANZA KUTUMIKA KWA SHERIA ZA HUDUMA ZA HABARI NA KANUNI ZAKE.
(Picha na Benedict Liwenga-WHUSM)
Na: Lilian Lundo–Dodoma
Waziri wa Habari
Utamaduni Sanaa na Michezo, Nape Nnauye ametanga rasmi kuanza kutumika kwa
Sheria ya Huduma za Habari ya mwaka 2016 na kanuni zake za mwaka 2017.
Nape Nnauye ametoa
taarifa hiyo leo katika ukumbi wa Bunge, Mjini Dodoma alipokuwa akiongea na
vyombo vya habari juu ya kuanza kwa sheria hiyo na kanuni zake.
“Kwa mujibu wa
kifungu cha 1 cha Sheria hiyo, ili ianze kutumika rasmi, Waziri wa Habari
anatakiwa kuitangaza tarehe ya kuanza kutumika, hivyo napenda kuufahamisha Umma
kuwa sheria hii imeanza kutumika tangu Desemba 31, 2016,” alifafanua Nape
Nnauye.
Aliendelea kwa kusema
kuwa kuanza kutumika kwa sheria hii ni jambo muhimu sana kwa tasnia hiyo kwa
sababu inaihamisha taaluma ya habari kutoka fani ambayo mtu yeyote anaweza
kujinasibu nayo hadi kuwa taaluma kamili yenye sifa mahsusi, maadili
yanayojulikana pamoja na vyombo vya kusaidia kusimamia utekelezaji wake.
Vile vile amesema
kuwa, sheria hiyo inaleta mfumo madhubuti wa kulinda haki za wanahabari kukusanya,
kuhariri na kusambaza habari zao kwa uhuru.
Pia sheria hiyo
imeweka wajibu kwa wale watakaokiuka misingi na maadili ya taaluma hiyo, hivyo
ukurasa mpya wa haki na wajibu umefunguliwa kupitia sheria hiyo.
Aidha amesema kuwa,
Wizara imechambua maoni mbalimbali kuhusiana na sheria hiyo ambapo moja ya
maoni hayo ilikuwa ni kiwango cha elimu cha mtu atakayeruhusiwa kufanya kazi ya
taaluma hiyo. Ambapo wapo waliopendekeza
kiwango cha elimu kiwe cheti, wengine diploma, digrii na hata PhD na wengine
walitaka awe mtu yeyote anayejua kusoma na kuandika.
Amesema kuwa Serikali
imesimama katikati ya maoni hayo, na sifa ya chini kabisa kwa kuanzia itakuwa
ni Diploma ya uandishi wa Habari. Hivyo Serikali imetoa kipindi cha miaka
Mitano kuanzia Januari, 01, 2017 kwa waandishi ambao hawana sifa hizo
kujiendeleza na kufikia kiwango hicho cha elimu.
Hivyo basi, Idara ya
Habari MAELEZO itaendelea kutoa “Press Card” bila kuwabana wanahabari kwa kuangalia
vigezo hivi vya kitaaluma bali dhamana ya waajiri wao.
Sheria ya Huduma za
Habari, 2016 ilisainiwa na Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli Novemba 16, 2016
na kuchapishwa kwenye gazeti la Serikali Novemba 18, 2016.