TIGO YAZINDUA TWENDE APP KUSAIDIA HUDUMA YA USAFIRI WA TEKSI NCHINI TANZANIA.
Mkuu wa Zana za Kidijitali wa Kampuni
ya Simu ya Tigo, Tawonga Mpore (kushoto), akizungumza katika mkutano na
waandishi wa habari Dar es Salaam leo, kuhusu kampuni hiyo kuzindua
Twende APP kwa ajili ya kusaidia huduma ya usafiri wa teksi nchini.
Kulia ni Mkuu wa Utawala na Fedha wa DTBi ambao ni wawezeshaji wa mradi
huo, Mramba Makange na Mkurugenzi wa Idara ya Ubunifu wa Costech,
Dk.Digushilu Mafunda.
Ofisa Mtendaji na Muasisi wa Twende App, Justin Kashaigili, akielezea jinsi ya kutumia mfumo huo kupitia simu ya mkononi.
Mkurugenzi wa Idara
ya Ubunifu wa Costech, Dk.Digushilu Mafunda (katikati), akizungumza
katika mkutano huo kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa Costech, Dk Hassan
Mshinda.
Wadau mbalimbali na waandishi wa habari wakiwa
kwenye uzinduzi huo.
Wapiga picha wakichukua tukio hilo.
Uzinduzi ukiendelea. |
Na Dotto Mwaibale
KAMPUNI inayoongoza kwa maisha ya
kidijitali Tigo Tanzania leo imezindua huduma mpya ya kidijitali
inayoitwa Twende App ambayo ni suluhisho la kuita teksi na hivyo
kuwapatia wateja wake huduma sahihi na wanayoimudu ya usafiri wa teksi
nchini Tanzania.
Kwa kuunganishwa moja kwa moja na
madereva wa teksi, huduma hiyo inawawezesha watumiaji kufurahia kiwango
cha chini kuliko ambavyo wangetumia njia nyingine mbadala za mitaani.
Twende App itakuwa na mawasiliano ya madereva teksi, bajaj na boda boda
ambao wamehalalishwa na vyama husika vya madereva.
Akitangaza huduma hiyo mpya katika
mkutano wa wanahabari jijini Dar es Salaam leo asubuhi , Mkuu wa Zana za
Kidijitali wa Tigo Tawonga Mpore alisema, “Huduma hii ni kielelezo cha
Tigo kujikita katika mageuzi ya mtindo wa maisha ya kidijitali kwa
kutoa suluhisho kwa changamoto zinazowakabili wateja wake. Tunaamini
kwamba Twende App itatoa huduma nzuri kwa abiria kwa kuwaunganisha na
madereva ambapo watapata huduma bora zilizo na gharama nafuu na zenye
ufanisi wa hali ya juu.”
Mpore aliongeza: “Tunaamini kwa kutoa
njia mbadala kwa usafiri uliopo wa teksi, tunaweza kusaidia kuboresha
usafiri kwa ujumla nchini Tanzania. Tunafahamu msongamano wa vyombo vya
usafiri uliopo jijini kwa sasa; hivyo tunalenga kuwa sehemu ya
suluhisho katika kutatua adha hiyo.
Kimsingi tunaamini kupunguza
usumbufu katika barabara za jijini na kupunguza athari za kimazingira
zinazotokana na msongamano wa magari ikiwa ni sehemu ya kukua kwa
uchumi.”
Uzinduzi huo pia ulihudhuriwa na
Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), Dk.
Hassan Mshinda ambaye alisema: “Napenda kumshukuru mbia wetu Tigo ambaye
kila mara amekuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha wajasiriamali
wetu vijana katika teknolojia ya kisasa wanapata msaada muhimu katika
kufikia malengo yao na kwa huduma hii naamini itawapatia fursa mpya
zenye manufaa kwa madereva kote jijini.”
Akizungumza wakati wa uzinduzi,
Ofisa Mtendaji na muasisi wa Twende App, Justin Kashaigili alisema:
“Nimesukumwa na kasi ya maendeleo ya miundo mbinu na nguvu ya
ujasiriamali hapa nchini. Ninategemea kuwapatia wakaazi wa jiji la Dar
es Salaam chaguo wanalolimudu, rahisi na linalofaa kwa ajili ya usafiri
salama.”
Akielezea jinsi ya kujiunga na huduma
hiyo, Kashaigili alisema, “abiria analotakiwa kufanya ni kupakua Twende
App katika simu yake ambayo itamuunganisha na dereva moja kwa moja
badala ya kuhangaika kwenda mwenyewe kufuata sehemu ilipo teksi.
Huduma hii pia inatumia muda sahihi wa taarifa za dereva, mfumo hai wa
satelaiti unaowezesha ramani ya kufahamu sehemu alipo abiria na
kumuunganisha abiria mwenyewe na dereva aliyepo karibu na wakati huo huo
kumwezesha dereva kutoa majibu.”
Twende App hivi sasa inatoa mbadala
sahihi wa malipo kupitia Tigo Pesa kwa namba binafsi za Tigo Pesa kwa
madereva na inapatikana katika mfumo wa Android na hivi karibuni
itapatikana kwa watumiaji wa simu zilizo na mfumo wa iOs.
(Imeandaliwa na mtandao wa www. habari za jamii.com-simu namba 0712-727062)