SERIKALI YAWAONDOA HOFU WANANCHI JUU YA HALI YA UPATIKANAJI WA CHAKULA NCHINI.
Na
Jacquiline Mrisho
SERIKALI imesema kuwa hali ya upatikanaji wa
chakula nchini ni ya kuridhisha na kuwataka wananchi kupuuza taarifa zinazodai
kuwa hali ya chakula ni mbaya.
Hayo yamebainishwa leo jijini Dar es Salaam na
Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi Dkt. Charles Tizeba wakati akizungumza na
waandishi wa habari kuhusu hali ya upatikanaji na chakula nchini.
“Ndugu waandishi ukweli ni kwamba hali ya
upatikanaji wa chakula nchini ni ya kuridhisha sana katika maeneo mengi, hivyo
siyo kweli kwamba kuna tatizo la njaa kama baadhi ya watu wanavyojaribu
kupotosha,” alisisitiza Dkt. Tizeba.
Aidha Dkt. Tizeba aliongeza kuwa pamoja na kuwepo
kwa hali nzuri ya chakula, Serikali kupitia Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya
Chakula (NFRA) imeendelea kuweka akiba ya chakula kwa kununua jumla ya tani 62,087.997 za mahindi ili kuhakikisha nchi inaendelea kuwa na
chakula cha kutosha.
Dkt. Tizeba amesema kuwa kwa mwaka wa fedha
2016/2017 Serikali imejipanga kununua
jumla ya tani 100,000 za chakula ambapo hadi kufikia Januari 8 mwaka 2017 imenunua jumla ya
tani 62,087.997 za mahindi sawa na asilimia 62 ya lengo ililojiwekea.
“Kati ya kiasi kilichonunuliwa, tani 38,162.280
zimenunuliwa kupitia vituo vya ununuzi na tani 23,925.717 kupitia vikundi vya wakulima hivyo hadi kufikia tarehe
12 Januari, 2017 Wakala wana akiba ya tani 88,152.443 za mahindi,” alisema Dkt. Tizeba.
Waziri Tizeba ameongeza kuwa hadi kufikia katikati
ya mwezi Januari, 2017 hali ya chakula na upatikanaji wake hapa nchini bado ni
ya kuridhisha na hasa upatikanaji wa vyakula kama mchele na maharage
ikilinganishwa na zao la mahindi.
Aidha, Wizara kwa kushirikiana na
Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI, FAO, TFNC pamoja na wadau wengine wanaendelea
kufanya tathmini ya kina ya hali ya chakula na lishe nchini ambayo inatarajiwa
kukamilika Januari 28 mwaka 2017 na itazihusisha Halmashauri 55, tathmini hiyo itaiwezesha
Serikali kupata taarifa za uhakika zaidi kuhusu hali ya chakula na lishe
nchini.
Amefafanua kuwa kutokana na hali ya mwenendo
wa unyeshaji wa mvua za vuli na msimu kutokuridhisha katika maeneo mengi ya
nchi, Serikali imewashauri
wakulima kutumia mbegu zitakazokomaa mapema na kupanda mazao yanayostahimili
ukame pamoja na kutumia kwa uangalifu na kuhifadhi akiba ya chakula cha kutosha
kwa matumizi katika kaya.
Aidha, Sekta binafsi zimehamasishwa kuendelea
kushiriki katika kutoa masoko ya kununua na kuuza mazao katika maeneo yenye
ziada na kuyauza katika maeneo yenye uhaba.
Ufafanuzi huo umetolewa kufuatia kuwepo kwa
taarifa za upotoshwaji juu ya hali ya upatikanaji wa chakula hapa nchini ambapo
Dkt. Tizeba amesema huo ni upotoshaji wenye lengo la kuwatia hofu wananchi.