Picha: MGODI WA BUZWAGI WAZINDUA KAMPENI YA WAKIA MOJA MTI MMOJA,MITI MILIONI 1.6 KUPANDWA KAHAMA

Mgodi wa dhahabu wa Acacia Buzwagi uliopo wilayani Kahama mkoani Shinyanga umezindua kampeni 'Wakia Moja Mti Mmoja' ikiwa na lengo la kupanda mti mmoja kwa kila wakia ya dhahabu iliyochimbwa kwenye mgodi huo matarajio yakiwa ni kupanda miti milioni 1.6 wilayani Kahama.


Akizungumza wakati wa uzinduzi wa Kampeni ya Wakia Moja Mti Mmoja, Meneja mkuu wa mgodi wa Acacia Buzwagi Mhandisi Asa Mwaipopo alisema mgodi huo ni wadau muhimu wa mazingira hivyo wanalojukumu la moja kwa moja kuhakikisha shughuli za utunzaji mazingira zinakuwa sehemu ya maisha ya kila siku.
Mhandisi Mwaipopo alisema kampeni hiyo ya upandaji miti itakayodumu kwa muda wa miaka miwili inayofadhiliwa na mgodi huo inalenga kuipendezesha wilaya ya Kahama sambamba na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia ya nchi.
Alisema zaidi ya shilingi milioni 645 zinatarajiwa kutumika katika awamu ya kwanza ya upandaji miti laki 5.
“Leo tunazindua awamu ya kwanza ya kampeni hii ambayo itahusisha upandaji wa miti 500,000,mpaka sasa miti 20,000 imekwisha pandwa na tunatarajia mpaka mwisho wa mwaka huu awamu ya kwanza ya miti 500,000 itakuwa imeshapandwa”,aliongeza Mwaipopo.
Alisema kupitia mipango yao ya muda mrefu uongozi wa mgodi huo umejiwekea lengo la kupanda mti mmoja kwa kila wakia moja ya dhahabu itakayokuwa ikizalishwa katika kipindi chote cha uhai wa mgodi huo ambapo inakisiwa mpaka mpaka shughuli za uzalishaji zitakapositishwa takribani wakia milioni 1.6 zitakuwa zimezalishwa.
Kwa upande wake mgeni rasmi wakati wa uzinduzi huo Mkuu wa wilaya ya Kahama Fadhili Nkurlu aliupongeza mgodi huo kwa kuona umuhimu wa kutunza mazingira na kwamba wanaunga mkono kwa vitendo jitihada zinazofanywa na serikali katika kupiga vita athari za tabia ya nchi.
“Naushukuru mgodi huu kwa kuunga mkono jitihada za serikali za kupanda miti kuhifadhi mazingira,serikali ina mpango wa kupanda miti katika kila halmashauri ili kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi na kuepusha nchi hii kuwa janga”,alieleza Nkurlu.
“Hatua iliyofanywa na wenzetu wa Buzwagi ni ya kizalendo,itasaidia katika kuboresha hali ya mazingira ya wilaya yetu,hili jukumu la kupanda miti ni letu sote,hatuna budi kuwaunga mkono kwa kuhakikisha kila mmoja wetu katika eneo lake anapanda miti na kuifanya wilaya yetu izidi kupendeza.
Aidha alitaka zoezi la upandaji miti liwe endelevu na kuiasa jamii kutunza miti hiyo na siyo kupitishia mifugo yao kwani itasababisha kuharibu miti iliyopandwa.
Na Kadama Malunde- Malunde1 blog
Meneja mkuu wa Mgodi wa Acacia Buzwagi Mhandisi Asa Mwaipopo akizungumza wakati wa uzinduzi wa Kampeni ya Wakia Moja Mti Mmoja iliyoanzishwa na mgodi huo lengo likiwa ni kupanda miti milioni moja na laki sita wilayani Kahama.Kulia ni Mkuu wa wilaya ya Kahama Fadhili Nkurlu,Kushoto ni Katibu Tawala wa wilaya ya Kahama Timoth Ndanya.
Mkuu wa wilaya ya Kahama Fadhili Nkurlu akizungumza wakati wa uzinduzi wa kampeni ya Wakia Moja Mti Mmoja
Mkuu wa wilaya ya Kahama Fadhili Nkurlu akipanda mti wakati wa uzinduzi wa Kampeni ya Wakia Moja Mti Mmoja
Mkuu wa wilaya ya Kahama Fadhili Nkurlu akimwagilia mti baada ya kuupanda

Meneja Mkuu wa Mgodi wa Buzwagi Mhandisi Asa Mwaipopo akijiandaa kupanda mti wakati wa uzinduzi wa kampeni ya Upandaji miti milioni moja na laki sita inayofadhiliwa na Mgodi wa Acacia Buzwagi ikiwa na lengo la kuufanya mji wa Kahama kuwa mzuri pamoja na kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabia ya nchi.

Meneja Mkuu wa Mgodi wa Acacia Buzwagi Mhandisi Asa Mwaipopo akijiandaa kuchukua udongo ili aweke kwenye shimo la mti
Meneja Mkuu wa Mgodi wa Acacia Buzwagi Mhandisi Asa Mwaipopo akimwagilia mti baada ya kuupanda
Mkuu wa kituo cha Polisi wilaya ya Kahama Musa Mchenya akipanda mti
Afisa Uendelevu katika mgodi wa Acacia George Mkanza akijiandaa kupanda mti
Meneja mkuu wa Mgodi wa Acacia Buzwagi mhandisi Asa Mwaipopo (kushoto) akiteta jambo na Mkuu wa wilaya ya Kahama Fadhili Nkurlu baada ya uzinduzi wa kampeni ya Wakia Moja Mti Mmoja
Wafanyakazi wa Mgodi wa Acacia Buzwagi wakimwagilia maji miti iliyopandwa na wengine wakiendelea kupanda miti
Zoezi la kuchimba mashimo kwa ajili ya kupanda miti likiendelea
Afisa Mawasiliano Mgodi wa Buzwagi Magesa Magesa akimwagilia maji mti alioupanda
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano katika mgodi wa ACACIA Buzwagi Blandina Munghezi akimwagilia mti baada ya kuupanda.Kushoto ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Musa Zeze Lutego Environmental Care akiwa ameshikilia mti akijiandaa kuupanda
Kitalu cha miche ya miti kinachotunzwa na Bwana Musa Zeze Lutego ambaye ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Lutego Environmental Care.Kitalu hiki kina jumla ya miche 570,000. Hapa ndipo miche kwa ajili ya kampeni ya Wakia Moja Mti Mmoja ya Acacia Buzwagi inatolewa kwa ajili ya kupandwa wilayani Kahama
Kitalu kikiwa na miche mbalimbali ya miti ya asili
Picha zote na Kadama Malunde-Malunde1 blog

Powered by Blogger.