MWENYEKITI WA CHADEMA ATUPWA JELA MIEZI MINANE BILA FAINI
VIONGOZI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) akiwemo Kaimu
Mwenyekiti wa Mkoa wa Lindi na Mgombea Ubunge wa Jimbo la Mtama,
Selemani Mathew na Katibu wa Chadema Kijiji cha Nyangamara ‘A’ mjini
Lindi, wamehukumiwa kifungo cha miezi minane jela bila ya faini kutokana
kufanya mkutano bila ya kibali cha Jeshi la Polisi katika kijiji hicho
wilayani Lindi.
Viongozi hao waliohukumiwa ni kati ya viongozi sita waliokamatwa na
kutuhumiwa kufanya mkutano bila ya kibali cha Jeshi la Polisi nchini.
Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi mkoani Lindi, Muhini alitoa
hukumu hiyo baada ya kusikiliza mashtaka pande zote mbili na kubaini
viongozi hao walitenda kosa la kisheria.
Tukio lililotokea Aprili 3, mwaka jana kwa viongozi na wanachama kwa
pamoja kufanya mkutano bila ya kibali cha Jeshi la Polisi wilayani
Lindi.
Alitaja kifungu cha sheria kilichovunjwa ni Kipengele 74(1) na 75
kinachozungumzia Mwenendo wa Makosa ya Jinai kinachosomeka kwa pamoja na
sheria ya Jeshi la Polisi.
Alisema washitakiwa wengine wanne wanaachiwa huru, kwani walibainika
hawana hatia. Hao ni Bashiru Rashidi, Hassani Mchilima, Abdallah
Mmasikini na Isimael Kupilila.
Akizungumzia hukumu hiyo, Mratibu wa Wanawake wa Chadema Mkoa wa Lindi,
Sina Kikuwi alisema mahakama haikutenda haki kwa watuhumiwa hao.
Alisema taarifa walikuwa nayo kwenye vikao hivyo vya ndani havihitaji
kibali, bali kutoa taarifa ambazo zilishatolewa katika mamlaka husika.
Selemani Mathew aliwahi kuwa Diwani wa Vijibweni wilaya ya Kigamboni
jijini Dar es Salaam kwa tiketi ya CCM. Aligombea katika Jimbo la Mtama
mkoani Lindi mwaka juzi, ambapo katika kura za maoni za CCM alishindwa
na Nape Nnauye.
Baadaye alihamia Chadema ambako alikuwa mgombea ubunge wa chama hicho,
lakini pia alishindwa na Nape ambaye sasa ni Waziri wa Habari,
Utamaduni, Sanaa na Michezo.