Waziri wa Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa (Wa pili kulia) akisikiliza
maoni kutoka kwa wateja waliotembelea kituo cha huduma kwa wateja cha Kampuni
ya Simu Tanzania (TTCL) ili kujipatia huduma zitolewazo katika duka hilo.
Picha na: Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
Waziri
wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa ameziagiza Taasisi
zote za Serikali nchini kuhakikisha zinaleta taarifa zao kuhifadhiwa katika
kituo cha Taifa cha Kuhifadhi kumbukumbu cha Kijitonyama (IDC) kwani kituo
hicho ni salama na kina ubora wa hali ya juu katika Kanda ya Afrika Mashariki
na Kati.
Aidha,
amezitahadharisha baadhi ya Taasisi zenye mpango wa kujenga na kuanzisha vituo vyao vya kuhifadhi kumbukumbu
kuacha mara moja mpango huo, kwani
kufanya hivyo ni kuingilia kazi ya kituo hicho na kupoteza fedha za Serikali.
Hayo
yamezungumzwa jijini Dar es salaam na Waziri huyo mara baada yakutembelea
kituoni hapo na kupokea taarifa ya uendeshaji wa kituo hicho kutoka kwa Mkuu wa
Kituo.
“Sioni
sababu kwa Taasisi nyingine kutaka kujenga vituo vyao vya kuhifadhi kumbukumbu,
Serikali imeshawekeza fedha nyingi kwa ajili ya ujenzi wa kituo hiki, hivyo
taasisi zote nchini zinalazimika kutumia kituo hiki”, amesema Profesa Mbarawa.
Sambamba
na hilo amezisisitiza kampuni zilizo chini ya Wizara yake kuwa mfano wa kuigwa
na taasisi nyingine nchini kwa kuwa wa kwanza kuleta taarifa zao kuhifadhiwa
katika kituo hicho.
Kwa
upande wake, Mkuu wa Kituo hicho Abdul Mombokaleo, amefanunua kuwa hadi sasa
wameshafanikiwa kuunganisha wateja 13 kujiunga na kituo hicho na wengine zaidi
ya 40 wapo katika mchakato wa kujiunga.
Katika
hatua nyingine, Waziri Mbarawa ametembelea ofisi za Kampuni ya Simu Tanzania
(TTCL) na kusema kuwa ameridhishwa na utendaji wa kampuni hiyo kutokana na
jitihada zake za kuteka soko la ushindani katika makampuni ya mawasiliano
nchini.
“Nimefarijika
zaidi kuona sasa TTCL inafanya vizuri katika eneo la masoko kwani nimeshuhudia
matangazo mengi barabarani, kwenye luninga, magazetini na katika mitandao ya
kijamii, hii inadhihirisha sasa mna mpango wa kuifufua kampuni hii”, amefafanua
Profesa Mbarawa.
Ameutaka
uongozi wa kampuni hiyo kuwa wabunifu na kufanya kazi kwa uadilifu na
ushirikiano ili kuleta mabadiliko chanya yatakayoboresha kampuni hiyo na kuteka
zaidi soko la mawasiliano nchini.
Imetolewa
na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano.
|