POLISI MARA HAISHIKIKI FA

Straika wa Rhino Rangers,Mansoul Ally akiwania mpira dhidi ya Moses Said Polisi Mara  katika mchezo wa kombe la FA uliofanyika katika uwanja wa Karume mjini Musoma juzi jumapili. katika mchezo huo polisi Mara walishinda 2-0
Mlinda mlango wa Polisi Mara Hasan Robert akiondoa kwa ngumi mpira eneo la hatari wakati wa mchezo wa kombe la FA uliofanyika juzi dhidi ya Rhino Rangers ya Tabora katika uwanja wa karume mjini Musoma. katika chezo huo Polisi Mara walishinda 2-0.

POLISI Mara imetamba nyumbani kwa kuitandika Rhino Rangers mabao 2-0 ligi ya F.A kwenye mchezo uliofanyika  jumapili katika Uwanja wa kumbukumbu ya Karume mjini hapa.
Bao la kuongoza la polisi Mara liliwekwa kimiani dakika ya 37 na Bauba Matagi na kuufanya timu hizo kuanza kushambuliana kwa kasi hadi mapumziko polisi Mara ilikuwa ikiongoza kwa bao 1-0.
Katika kipindi cha pili timu zote zilianza mashambulizi ya hapa na pale kwa zamu na hadi dakika ya 78 Polisi Mara iliongeza bao la pili kupitia kwa Moses Said aliyekuwa ameingia dakika mbili zilizokuwa zimepita.

Bao la pili la Polisi Mara liliwafanya mashabiki na viongozi wa timu hiyo kunyanyuka kwenye viti vyao kuonyesha furaha ya kupata ushindi huo.

Kocha mkuu wa Polisi Mara, Henry Mkanwa alisema kikosi chake kinaendelea kuimarika siku hadi siku kutokana na kazi kubwa anayoifanya ya kukinoa.

Alisema wadau wa soka mkoani mara wategemee kuona timu hiyo ikiimarika zaidi katika michuano ya ligi daraja la kwanza hasa ikifanya vizuri zaidi musimu ujao.

“Hatutashuka daraja kama ilivyokuwa inasemwa na wadau na mashabiki wetu baada ya kufanya vibaya katika mzunguko wa kwanza na mwanzo wa huu wa pili,”alisema Mkanwa.  

Kocha wa viungo wa Rhino Rangers, Dan Murumbe alikubaliana na ushindi wa Polisi Mara huku akisema makosa yaliyofanywa na mabeki wa timu yake ndiyo yaliyoigharimu.

“Ushindi ulikuwa wa halali, tumetolewa F.A kutokana na mfumo uliopo wa ukipigwa unatoka, nasi tumetoka tunaenda kujiandaa na ligi daraja la kwanza,”alisema Murumbe.

Akizungumza kwa niaba ya mashabiki wa Polisi Mara, Khalid Opec alisema timu hiyo imeanza kurudisha mashabiki wake na itafikia malengo ya mkoa kuwa timu bora.

“Kwa sasa tunaona Polisi Mara inaanza kutuonyesha kuwa makocha wanafanya kazi, chama cha soka na ofisi ya mkoa maleno yao yaweza kutimia kuiinua timu hii,”alisema Opec.
Mwisho.
 



Powered by Blogger.