JINSI KAULI NZITO YA RAIS MAGUFULI ILIVYOWAVURUGA WADAU WA HABARI TANZANIA
SAA chache baada ya Rais Dk. John
Magufuli kusema kuna magazeti mawili siku zake zinahesabika kutokana na
kuandika habari za uchochezi, mjadala mkubwa umeibuka huku wadau wa
habari wakitoa maoni yao kutokana na kauli hiyo.
Mjadala huo ulioibuka katika mitandao ya
kijamii ulibebwa na maswali kadhaa ikiwamo majina ya magazeti na habari
zipi yaliyoandika ambazo ni za uchochezi.
Akizungumza mjini Shinyanga jana
alipofungua viwanda vya Jambo Food Products Co. Ltd kinachojihusisha na
uzalishaji wa vinywaji na Fresho Investment Co. Ltd kinachojihusisha na
uzalishaji wa vifungashio vya mazao, alisema Serikali yake haitasita
kuyafuta magazeti mawili ambayo hakutaja majina kwa sababu ya habari
hizo zinazoweza kusababisha uvunjifu wa amani.
“Navipongeza vyombo vyote vya habari kwa
kazi nzuri ya kuhabarisha Watanzania isipokuwa magazeti mawili tu
ambayo yenyewe kila siku ni kuandika habari za uchochezi tu, bahati
nzuri Watanzania wanayajua na wamekuwa wakipuuza habari zao, wao
ukizungumza neno wanageuza neno hili, ukizungumza habari hii wao
wanageuza hivi.
“Magazeti haya mawili siku zao
zinahesabika, huo ndio ujumbe, wasifikiri wanafanya tunawaangalia,
Serikali ya kutumbua majipu haiwezi kuacha kutumbua magazeti yanayofanya
kazi ya kuchochea, kama wanasikia wasikie, kama hawasikii wasisikie,”
alisema.
Magufuli alisema kamwe hatakubali amani
ya nchi ivurugwe na vyombo hivyo vya habari ambavyo vimekuwa vikitumiwa
vibaya na baadhi ya wanasiasa.
Pia alisema hata mauaji ya Kimbari
yaliyotokea Rwanda mwaka 1994 yalisababishwa na baadhi ya vyombo vya
habari baada ya kuandika taarifa za uchochezi.
“Tanzania ni kimbilio la nchi nyingine,
kamwe sitakubali nchi ivurugwe na vyombo vya habari vichache ambavyo
kazi yao kila kukicha ni kuandika habari za uchochezi, amani ni kitu
kikubwa, wanaomwamini Yesu Kristo kuna maneno alisema amani nawaachieni,
amani ni kitu muhimu sana.
“Magazeti mengine yanafanya kazi vizuri
sana, isipokuwa haya mawili tu, naombeni tufanye kazi uchaguzi umeisha,
mimi kama rais wenu nitaendelea kulinda amani ya nchi hii, wanaochochea
hawataki tuwe na amani, hawataki tuwe na viwanda,” alisema.
Baada ya Magufuli kuzungumza hivyo,
wadau wa tasnia ya habari walizungumza na MTANZANIA Jumamosi kwa njia ya
simu jana na kutoa maoni tofauti.
PROFESA BANA
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam
(UDSM), Profesa Benson Bana, aliichambua kauli hiyo kwa kusema Magufuli
ashauriwe kuhusu habari ili awe mvumilivu wa baadhi ya mambo.
Alisema kwa mtazamo wake hatarajii
magazeti yote yaandike akitakacho Magufuli kwa sababu magazeti mengine
yanapima mauzo ya habari na sera zao.
“Nadhani hili suala linahitaji uvumilivu
zaidi wa mawazo na fikra tofauti. Ndiyo uhuru wa watu kuandika
wakitakacho, kusema wakitakacho ili mradi wasivunje sheria. Kuna
magazeti ambayo yapo upande wa Serikali na mengine yanakosoa Serikali,
hayo ndiyo mambo ya kuvumiliana.
“Nadhani Rais ashauriwe vizuri kwamba
aweze kuwa mvumilivu kwa baadhi ya mambo kwa sababu huo ndio uhuru wa
habari kama rais anaona magazeti yanakwenda kinyume sheria zipo,”
alisema.
Pia alisema tangu wakati wa uchaguzi uliopita magazeti mengi yamekuwa na misimamo yake kutokana na mazingira yaliyokuwapo.
“Nadhani unajua unakuta misimamo fulani
kwa maana ya gazeti fulani, habari fulani ya mtu fulani ikapewa uzito
hata kama alivyosema vinastahili kuhojiwa kiuandishi, lakini vikapewa
uzito ndiyo habari yenyewe.
“Sasa hiyo rais na Serikali yake
hawawezi kuingilia haraka haraka labda kama kuna gazeti limekiuka
maadili, sheria za nchi hapo sawa. Lakini hii ya kuchukua misimamo na
kuandika wanachofikiri ni sahihi na hilo nadhani ni gumu kwa rais
kuliweka wazi isipokuwa ni kuelimishana tu kwamba unaandika kwa faida
gani na unaandika kwa faida ya nani na kwanini uchukue msimamo,”
alisema.
TEF
Naye Katibu wa Jukwaa la Wahariri
Tanzania (TEF), Neville Meena, alisema Magufuli amekwenda mbali kwa
kutoa kauli hiyo kwa sababu yeye kama mkuu wa nchi magazeti mawili si
saizi yake.
Alisema rais anatumia nguvu kubwa pasipo
uhitaji: “Ukiwa mkuu wa nchi ukaanza kushugulika na gazeti moja au
mawili haileti maana kwa sababu rais unaweza kuzungumza kwa ujumla
kuhusu vyombo vya habari vya nchi, lakini hatari yake kwa sasa hivi
mambo yanaweza kutokea kwa maana ya watu wanaweza kutokea wenye nia
mbaya wakashughulikia vyombo vya habari kwa kutumia kigezo cha kwamba
kauli ya rais ni amri.
“Lakini pia chombo hicho cha habari kitakachoguswa sasa hivi kitajua kwamba rais ndiye kaelekeza kishughulikiwe,” alisema.
Aliongeza kwamba, nchi inaendeshwa kwa
mujibu wa sheria na sheria za habari zipo na zimewekwa kwa mtu yeyote
akiwamo rais mwenyewe.
“Sasa kwa kauli kama hiyo rais
ameshavihukumu vyombo vya habari hata kabla ya kusikilizwa, hivyo
chochote kitakachotokea ni kwamba sijui itakuwaje, lakini inawezekana
rais ameshatoa maelekezo ya kwamba washughulikie hivyo vyombo ambavyo
hajavitaja,” alisema.
KIJO BISIMBA
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa
Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk. Helen Kijo-Bisimba,
alisema kauli ya Rais Magufuli inatishia Watanzania.
Alisema kama kuna magazeti hayafanyi
vizuri kwa mujibu wa sheria na taratibu zilizowekwa vyombo husika
vifuatiliwe na kuchukua hatua inavyostahili.
Bisimba alisema rais kutoa kauli hiyo
yenye fumbo ni kiashiria cha kutisha mawazo ya wananchi kwa sababu
taarifa za wananchi ndizo huzaa habari katika magazeti.
“Kwa mfano gazeti ukiachia tahariri,
mambo mengine ni sauti ya watu kwamba watu wanasema watu wanaandika,
hivyo ukitoa vitisho hivyo maana yake ni kuwatisha wananchi wasiuseme
ukweli, hata huo ukweli anaopenda kuutoa rais basi usiwafikie wananchi
kwa sababu waandishi watakuwa na hofu ya kuandika.
“Ifahamike vyombo vya habari haviwezi
kufanya vitu vyake pasipo kupewa taarifa kutoka kwa wananchi kwa mfano
kama hivi unavyoniuliza ni kwa sababu rais kasema, lakini kama
asingesema usingeniuliza,” alisema.
MCT
Katibu Mtendaji wa Baraza la Habari
Tanzania (MCT), Kajubi Mkajanga, alisema hawezi kutoa tamko rasmi
kuhusiana na kauli hiyo kwa sababu walikuwa katika kikao cha ndani
kuongelea mustakabali wa vyombo vya habari na hata kauli ya Magufuli ni
sehemu ya mjadala.
“Hilo tunalijadili kwa hiyo siwezi
kulitolea taarifa kwa sasa, lakini ninachotaka tu kusema ni vigumu
kutaka mimi kusema kitu cha moja kwa moja kwa sababu magazeti yenyewe
hayakutajwa wala habari hizo zinazosemekana ni za uchochezi
hazikubainishwa ni habari gani. Lakini kwa ujumla tamko hili lazima
litajenga hofu kwa waandishi na kwa wahariri kwa sababu mkuu wa dola
akitamka ina asili ya kujenga hofu,” alisema.
PROFESA SHIVJI
Mhadhiri Mstaafu wa UDSM, Profesa Issa
Shivji, alipoulizwa na gazeti hili kuhusu maoni yake juu ya kauli hiyo
alijibu kwa kifupi hana cha kusema.
Imeandikwa na Kadama Malunde, Shinyanga na Evans Magege- Dar es Salaam wa gazeti la Mtanzania