Na: Frank shija
WATAALAM wa mifupa wamepelekwa katika
Hospitali zote za Kanda na matarajio ya baadaye ni kuwapeleka katika Hospitali
za Mikoa ikiwa ni kusogeza huduma za tiba ya mifupa karibu zaidi na wananchi.
Hayo yamebainishwa na Katibu Mkuu wa
Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Mpoki Ulisubisya
katika kipindi cha TUNATEKELEZA kinachorushwa na kituo cha luninga cha TBC1 kwa
kushirikiana na Idara ya Habari MAELEZO jana jijini Dar es Salaam.
Dkt. Ulisubisya amesema kuwa wataalamu
hao wamepelekwa katika Hospitali hizo ili kutatua changamoto ya matibabu ya
magonjwa ya mifupo yaliyoongezeka kwa wingi kutokana na ajali hasa zitokanazo
na Bodaboda.
“Serikali imepeleka Wataalamu wa
mifupa katika Hospitali za Kanda ikiwa ni njia ya kusogeza huduma za matibabu
ya mifupa karibuzaidi na wananchi kwani kumekuwa naongezeko la wagonjwa
kutokana na ajali hasa za Bodaboda” alisema Dkt. Ulisubisya.
Aidha Katibu
Mkuu huyo amesema kuwa pamoja na kupeleka wataalamu wa mifupa katika Hospitali
za Kanda na mikoa, mikakati ya Serikali ni kuhakikisha huduma za Afya zinakuwa
bora na zinawafikia wananchi kwa urahisi ndiyo maana Serikali ya Awamu ya Tano
chini ya Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli imekuja na dhana ya kuwa na
Zahanati kila Kijiji ambazo zitapatia dawa na vifaa tiba muhimu.
Aliongeza kuwa
katika kuhakikisha dhana hiyo inatekelezeka Wizara ya Afya imekuwa
ikishirikiana na TAMISEMI ambayo ndiyo yenye jukumu la kusimamia huduma,
kuhakikisha huduma za msingi zinapatikana ikiwemo miundombinu ya Zahanati,
Vituo vya Afya na Hospitali pamoja na Dawa na Vifaa Tiba.
“Pamoja na
kuwa mambo mengine yanasimamiwa na TAMISEMI lakini ninapokuwa katika ziara
nikikutana na changamoto zinazowahusu nashughulikia kisha nawapa taarifa ili
wachukue hatua stahiki, hivyo ndivyo tunavyoshirikiana katika kuhakikisha
wananchi wanapata huduma bora za Afya.”Alifafanua
Kuhusu upatikanaji wa dawa Dkt.
Ulisubisya amesema kuwa hadi kufikia mwezi wa tano upatikanaji wa dawa utakuwa
umefikia asilimia 90% kutoka 70% za sasa na kuongeza kuwa suala la dawa
limepewa kipaumbele katika bajeti ya mwaka wa fedha wa 2016/2017 ambapo
takribani shilingi 251 bilioni zimetengwa kwa ajili ya dawa na vifaa tiba. |