Na: Frank Shija
Mwili wa aliyekuwa
Mgombea wa kwanza Mwanamke kuwania kiti cha Urais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Dkt. Anna Senkoro unatarajiwa kuzikwa katika makaburi ya Kinondoni
jijini Dar es Salaam siku ya jumamosi tarehe 07/01/2017 kuanzia saa 8:00 mchana.
Taarifa hiyo
imetolewa leo jijini Dar es Salaam na Bwana. Fred Sendim ambaye ni Msemaji wa
Familia ya marehemu Dkt. Senkoro.
“Mipango ya mazishi
inaendelea vizuri nyumbani kwake Segerea, pia nitumia fursa hii kutoa shukrani za
kipekee kwa wote wanaoendelea kutufariji na kushirikiana nasi bega kwa bega
katika kipindi hiki kigumu.” Alisema Sendim.
Msemaji huyo wa
familia amesema kuwa taratibu za mazishi zitataunguliwa na Ibada maalum
itakayoambatana na utoaji wa heshima za mwisho kuanzia saa Saba mchana katika Kanisa la Winners
lililopo Banana, Ukonga jirani na Kituo
cha Mafuta cha Oil Com.
Awali akielezea kifo
chake msemaji wa familia hiyo amesema kuwa marehemu alikuwa anasumbuliwa na
ugonjwa wa moyo ambapo juzi tarehe 04 majira
ya saa 11 alfajiri alizidiwa na kupelekwa Hospitali kwa ajili ya matibabu katika
Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) na baadaye alihamishiwa Hospitali ya
Taifa Muhimbili ambapo alifikwa na mauti mnamo saa 3:30 asubuhi.
Dr.Anna Senkoro
alikuwa mgombea wa kwanza mwanamke kuwania kiti cha Urais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania mwaka 2005 kupitia Chama cha APPT Maendeleo, Marehemu
ameacha watoto wa tatu na wajukuu wa wiwili.
Mungu ailaze roho ya Marehemu mahali pema
peponi amina.
|