Mkurugenzi wa halmashauri ya
mji wa Tarime mkoani mara, Elias Ntiruhungwa amemsimamisha kazi afisa utumishi
wa halmashauri hiyo kwa kosa la uzembe wa kutekeleza majukumu anayopewa.
Akitoa taarifa hiyo kwenye kikao cha
kazi na watumishi wa halmashauri ya mji wa Tarime alisema kuwa amefikia uwamuzi
huo kutokana na afisa utumishi huyo Jeveryson Kaguna kushindwa kutimiza
majukumu anayopewa na ofisi ya mkurugenzi kwa wakati.
Amesema kuwea kutokana na uzembe huo
amesababisha watumishi kuidai halmashauri hiyo kiasi kikubwa cha fedha na kuwa
tatizo hilo limewafanya wapoteze ari ya kufanya kazi.
“Unampa kazi na muda wa kuimaliza
kazi hiyo, hatekelezi muda unaisha na hatoi taarifa ya nini kimemfanya
asikamilishe kazi hiyo, kama huwezi kazi andika barua ya kuomba kuachia ukuu wa
kitendo ulicho nacho utaonekana wa maana kuliko kusubiria maamuzi kutoka juu,”
alisema Ntiruhungwa.
Aidha amemsimamisha kazi Muuguzi wa
hospitali ya mji wa Tarime Kegose Nega Jackson kwa kosa la kushindwa kutii
agizo la mkubwa wake wa kazi la kusukuma kitanda cha mgonjwa.
“Huu ni utovu wa midhamu na hatuwezi
kukubali tabia hii kuendelea, mwananchi wa kawaida hawezi kupeleka mgonjwa
hospitalini na kufanya kazi ya wataalamu,´alisema Ntiruhungwa.
Akizungumza katika kikao hicho
katibu tawala wa wilaya ya Tarime John Marwa amewaagiza watumishi wote wa
serikali kutekeleza wajibu wao kwa kuzingatia sheria na taratibu za kazi ili
kuepukana na matatizo yanayeoweza kuzuilika.
“Hakuna kiongozi anayemfukuza
mtumishi kazi bali mtumishi anajifukuzisha kazi mwenyewe kwa kushindwa kutimiza
wajibu,” alisema Marwa.
Wakizungumza katika kikao hicho
kilichojumuisha watumishi wa Elimu, Afya, watumishi wote wa idara katika
halmashauri ya mji wa Tarime, watumishi wameonyesha kufurahia hatua
iliyochukuliwa na mkurugenzi huyo.
“Huu ni wakati wa kuchapa kazi hatua
aliyoichukua mkurugenzi ni sahihi na inapaswa kuwa fundisho kwa wengine
tuliobaki, ukitimiza wajibu wako hakuna mtu atakayekugusa,” alisema Samson
Marwa.
|