WAZIRI WA NISHATI NA MADINI ATATUA MVUTANO BAINA YA TANESCO NA WASHIRIKA WAKE JIJINI MWANZA.
Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo (katikati), hii leo akizungumza na wanahabari baada ya kikao baina yake na viongozi
wa Tanesco pamoja na wawakilishi wa kampuni zilizohusika na
utengenezaji na ufungaji wa mitambo katika kituo cha kuzalisha umeme kwa
kutumia mafuta mazito cha Nyakato Jijini Mwanza.
Kushoto ni balozi wa Norway nchini
Tanzania, Hanne-Marie Kaarstad na kulia ni balozi wa Denimark hapa
nchini, Einar Jensen. Mabalozi hao wamehudhuria kikao hicho ikiwa ni
sehemu ya kusaidia kutatua mvutano baina ya kampuni zinazotoka katika
nchi zao na Tanesco kutokana na baadhi ya mitambo iliyofungwa na kampuni
hizo katika kituo cha Tanesco Nyakato Jijini Mwanza kuharibika. Mradi
huo uligharibu shilingi bilioni 129 hadi kukamilika kwake na una uwezo
wa kuzalisha Megawati 60 za umeme.
#BMGHabari
Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo (katikati), balozi
wa Norway nchini Tanzania, Hanne-Marie Kaarstad (kushoto) pamoja na
kulia ni balozi wa Denimark hapa nchini, Einar Jensen (kulia)
Waziri wa
Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo, ameliagiza Shirika la Umeme
nchini Tanesco kufanya matengenezo kwenye mitambo yake minne ya
kuzalisha umeme iliyoharibika katika Kituo cha Nyakato Jijini Mwanza
kabla ya kufikia Februari 28 mwakani.
Profesa Muhongo
ametoa agizo hilo hii leo Jijini Mwanza, baada ya kukutana na viongozi
wa Tanesco pamoja na wawakilishi wa kampuni zilizohusika na utengenezaji
na ufungaji wa mitambo hiyo kutoka nchi za Norway na Denmark ambapo pia
mabalozi wa nchi hizo wamehudhuria kikao hicho.
Aidha Profesa
Muhongo ameiagiza Tanesco kuhakikisha mitambo sita iliyosalia
haiharibiki tena na kwamba inamaliza kazi ya kusafisha mitambo yote
katika kituo hicho kabla ya kufikia mwezi Februari 28 mwakani ambapo
imeelezwa kwamba baadhi ya mapungufu katika mitambo hiyo yalitokana na
kutosafishwa kwa wakati. Kampuni zote mbili zimekubali kushirikiana na
Tanesco katika kutekeleza makubaliano hayo.
Awali kulikuwa
na mvutano baina ya Tanesco na Kampuni ya Rolls Royce ya nchini Norway
iliyotengeneza mitambo hiyo pamoja na kampuni ya Semco ya nchini Denmark
iliyofunga mitambo hiyo, baada ya mitambo minne kati ya 10 kuharibika
ndani ya kipindi cha miaka miwili na hivyo kusababisha uzalishaji wa
megawati 18 kati ya 60 zilizopaswa kuzalishwa kupungua.
Hata hivyo
pande zote zinazolalamikiana zimeonekana kuwa na hoja ambapo Profesa
Muhongo ameitaka Tanesco kuandika malalamiko yake na kuyawasilisha kwa
kampuni Rolls Royce iliyotengeneza mitambo hiyo kabla ya februari 28
mwakani, malalamiko ambayo yanapaswa kujibiwa hadi kufikia tarehe 30
mwezi Machi mwakani ili kujua maamuz yatayofuata.
Mabalozi wa
pande zote mbili, ambao ni Hanne-Marie Kaarstad kutoka nchini Norway
pamoja na Einar Jensen wa Denmark, wameeleza kuridhishwa na makubaliano
ya kikao hicho wakiamini kwamba mwafaka huo utasaidia uzalishaji wa
umeme kama ilivyokusudiwa ili kufikisha huduma ya umeme kwa wananchi.