CCM KUANZA KUTUMBUANA KUSAFISHA CHAMA...MATAJIRI WA HILA NDANI YA CCM KUFUKUZWA
Mabadiliko yaliyofanywa ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) yamekuja na
mkakati mpya wa kuwavua ‘gamba’ makada wa chama hicho wenye ukwasi
waliovuna kinyume na taratibu.
Katibu wa Halmashauri Kuu (NEC) Itikadi na Uenezi wa chama hicho,
Humphrey Polepole amesema kuwa wako katika mkakati wa kukisafisha zaidi
chama hicho, akiwataka matajiri wenye ‘makandokando’ wajiondoe mapema.
“Kuwa tajiri si dhambi na si kwamba CCM inafukuza matajiri, hapana.
Tatizo letu kama CCM katika mwelekeo mpya, mtazamo mpya na maegeuzi
yanayofanyika, hatuhitaji kuwa na aina ya matariji wanaojipatia utajiri
wao kwa hila, kwa rushwa na kwa dhuluma,” alisema Polepole katika
mahojiano na kituo kimoja cha runinga nchini.
“Ukijiona wewe ni tajiri na mikono yako ni michafu kwa maana ya kuwa na
makando ya kukosa uaminifu, hulipi kodi, ukae mbali na CCM,”aliongeza.
Alisema watawachukulia hatua za kuwaondoa ndani ya chama hicho na
kuwakabidhi kwa vyombo vya dola ili wachukuliwe hatua za kisheria.
Tangu alipochaguliwa, Polepole amekuwa akisisitiza kuwa chama hicho kitajikita katika msingi wake wa kuwatumikia wanyonge.
Mkakati huo wa kuwang’oa matajiri wasiowaaminifu ndani ya chama hicho
unafanana na oparesheni iliyobatizwa jina la ‘Vua Gamba’ ndani ya chama
hicho miaka kadhaa iliyopita, iliyolenga kuwang’oa viongozi na vigogo
ambao walibainishwa kujipatia mali kinyume cha utaratibu na mafisadi.