Inatisha!! MKULIMA ACHOMWA MKUKI MDOMONI,WATOKEZEA SHINGONI,ACHANIKA ULIMI
Inaelezwa kuwa Mtitu alikaa na mkuki huo kwa saa sita kabla ya kufanyiwa upasuaji uliochukua saa moja kuutoa.
Majeraha hayo yamemfanya Mtitu ashindwe kuongea kutokana na maumivu
makali baada ya kuathirika mfupa wa taya na kuchanika ulimi.
MKULIMA na mkazi wa kijiji cha Dodoma Isanga kata ya Masanze wilaya ya
Kilosa mkoani Morogoro, Augustino Mtitu,amechomwa mkuki mdomoni na
kutokea shingoni.
Umemjeruhi hivyo kulazimika kukimbizwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa
Morogoro, kufanyiwa upasuaji kuondoa mkuki huo na kuokoa maisha yake.
Mtitu na wengine wanane walijeruhiwa katika vurugu zilizohusisha jamii
ya wafugaji wa Kimasai na wakulima wa kijiji hicho kilichopo wilayani
Kilosa.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Morogoro, Ulrich Matei alithibitisha
kutokea kwa tukio hilo. Alisema mpaka jana watu watatu walikuwa
wanashikiliwa na Polisi, na msako unaendelea kuwasaka wale wote
waliohusika katika kufanya vurugu hizo.
Tukio hilo ni la Desemba 25, mwaka huu, baada ya mtu huyo kujaribu
kuzuia vurugu hizo, zilizokuwa zimetokea baada ya wafugaji hao kulisha
mifugo yao katika shamba la maharage na mahindi katika kijiji hicho.
Mtitu akijaribu kuzuia vurugu hizo, aliishia kuchomwa mkuki na mmoja wa
wafugaji wa jamii hiyo, ambao baada ya tukio hilo walikimbia kutoka eneo
hilo.
Kutokana na tukio hilo, wananchi wenzake waliamua kumkimbiza katika Hospitali ya Wilaya ya Kilosa kwa ajili ya matibabu.
Lakini, alihamishiwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro kwa ajili ya
kufanyiwa upasuaji na matibabu zaidi ya kuokoa maisha yake.
Baada ya kutokea kwa tukio hilo, muda mfupi baadaye wafugaji hao
walirudi tena kijijini hapo, kwa lengo la kuokoa mifugo yao iliyokuwa
imekamatwa, na ndipo walipoanzisha tena vurugu kwa kuwashambulia watu
wengi wanane akiwemo Mwenyekiti wa Kijiji pamoja na wa Kitongoji.
Watu watano, kati ya waliojeruhiwa, walikimbizwa katika Hospitali ya
Wilaya ya Kilosa kupatiwa matibabu. Diwani wa Kata ya Masanze, Bakari
Pilo, akizungumza kwa njia ya simu, alisema hilo ni tukio la tatu
kutokea kwenye kata yake katika kipindi kifupi.
Alisema vitendo hivyo vinaendelea kuhatarisha usalama wa wananchi, hasa
wakulima, kufuatia mamlaka zinazohusika kushindwa kuwahamishia wafugaji
katika eneo walilokuwa wametengewa, licha ya suala hilo kupitishwa
kwenye vikao vya Baraza la Madiwani.
Stanley Andrea, ambaye ni ndugu wa Mtitu, yupo katika Hospitali ya Rufaa
ya Mkoa wa Morogoro akimuunguza nduguye, alisema kuwa tukio hilo ni la
Desemba 25, mwaka huu majira ya saa 5 asubuhi kwenye mashamba ya
wakulima baada ya wafugaji kuingiza mifugo kwenye mashamba ya mahindi na
maharage ili kulisha mifugo.
Alisema, wakulima wenye mashamba hayo,waliamua kuifukuza mifugo hiyo,
lakini wafugaji wa jamii ya Kimasai, waliingilia kati na kuanza kuwapiga
kwa fimbo wakulima na kusababisha kutokea kwa vurugu baina ya pande
mbili hizo.
Alisema, mfugaji mmoja wa Kimasai alichukua mkuki na kumchoma Mtitu
sehemu ya mdomoni na kutokezea shingoni na kuwajeruhi wengine wanane,
akiwemo Mwenyekiti wa Kijiji na wa Kitongoji, ambao baadhi wamelazwa
Hospitali ya Wilaya ya Kilosa.
Alisema kuwa vurugu ziliongezeka, pale wafugaji hao waliporudi kijijini
hapo kwa ajili ya kuikomboa mifugo yao iliyokuwa inashikiliwa, kabla ya
kufika kwa askari polisi kutoka mjini Kilosa.
Muuguzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro, Sanifa Mdee, alisema
walimpokea mgonjwa huyo akiwa na mkuki mdomoni, ulitokea upande wa
shingoni na kuanza kumpatia matibabu na kumtoa mkuki huo, ambapo
amelazwa wodi namba moja hospitalini hapo.
Hata hivyo, alisema kutokana na mkuki huo kuchomwa kwa nguvu, ulijeruhi
baadhi ya meno yake na kuharibu fizi, hali iliyosababisha jana madaktari
kumfanyia upasuaji wa kurekebisha fizi zake, ambapo baada ya kutolewa
mkuki huo, hali yake ilikuwa inaendelea vizuri. Kamanda wa Polisi wa
Mkoa wa Morogoro, Ulrich Matei, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo.
Alisema mpaka jana watu watatu wanashikiliwa na Polisi, na msako
unaendelea kuwasaka wale wote waliohusika katika kufanya vurugu hizo.
Pia alisema majeruhi aliyechomwa mkuki, anaendelea kupatiwa matibabu
katika Hospitali ya Rufaa ya Morogoro na anaendelea vizuri, kama
anavyobainisha muuguzi aliyempokea mgonjwa huyo.
Kwa mujibu wa Kamanda Matei, mmiliki wa
mifugo iliyoingizwa katika shamba hilo, amekwishatambuliwa na anaendelea
kutafutwa, ili aweze kuwataja wachungaji wake, ambao ndiyo wanadaiwa
kumchoma mkuki Mtitu na kuwajeruhi wakulima wengine wanane.
Imeandikwa na John Nditi-Morogoro