TAARIFA KWA UMMA KUHUSU DAWA ZA KUTIBU SUMU YA NYOKA TANZANIA
Kama tunavyofahamu, nchi yetu ina aina mbalimbali za nyoka ambao pindi
wakimuuma mtu huleta madhara mbalimbali ya kiafya. Aidha tunafahamu
kwamba tatizo hili lipo zaidi katika maeneo ya vijijini ambako uwezo wa
wananchi kumudu gharama za matibabu ni mdogo.
Dawa za kutibu sumu ya nyoka huagizwa kutoka nje ya nchi. Dawa hizo siyo
tu hazipatikani kwa urahisi, bali pia zinapatikana kwa gharama kubwa.
Bei ya kununulia dawa hizi ni kati ya dola za kimarekani 55 hadi 85
(yaani shilingi za kiTanzania 118,250 hadi 182,750) kwa kichupa kidogo
(vial) kimoja. Kichupa hicho huweza kutumika kwa wagonjwa wanne, lakini
mara tu baada ya kufunguliwa dawa hiyo huwa haifai tena kutumika ndani
ya mwezi mmoja tu.
Pamoja na changamoto hizo, Serikali kupitia MSD kila mwaka huagiza dawa
hizi kwa ajili ya mahitaji hayo ya kutibu wagonjwa walioumwa na nyoka,
ambapo bei ya kuinunua kutoka MSD ni TZS 200,000/= kwa kichupa kimoja.
Hospitali zetu mbalimbali zimekuwa zikiagiza dawa hizi kutoka MSD na kwa
washitiri wengine kwa bei hii au zaidi na kuwatibu waathirika
wanaohitaji dawa za sumu za nyoka mara zinapohitajika.
Napenda kuwakumbusha kwamba kwa mujibu wa Sera ya Afya ya mwaka 2007,
huduma za tiba hutolewa bure kwa makundi maalum, au kwa kuchangiwa kwa
sehemu ya gharama, au kwa kupitia mfumo wa Bima mbalimbali za Afya kama
vile CHF. Kwa wale wasio na uwezo na wanaothibitishwa kuwa hawana uwezo,
utaratibu wa msamaha hutumika.
Katika kuhakikisha kwamba wananchi wanaohitaji dawa ya sumu ya nyoka
wanahudumiwa ipasavyo, Mhe. Ummy Mwalimu, Waziri wa Afya, Maendeleo ya
Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto anatoa maelekezo yafuatayo:-
Waganga Wakuu wa Mikoa na Viongozi wa Hospitali zote nchini wahakikishe
kuwa Hospitali zote za umma zinaingiza dawa hii katika dawa za dharura
ili iweze kununuliwa kama dawa zingine za dharura kupitia kifungu cha
fedha za dawa za dharura.
Kwa wagonjwa ambao watakuwa na Bima ya Afya, basi gharama za matibabu
hayo zitalipwa kwa kupitia utaratibu huo wa Bima. Wananchi wanahimizwa
kujiunga na Bima za Afya (CHF/NHIF) ili kupata unafuu wa matibabu haya
na mengine. Mfano CHF - gharama ya kujiunga katika Halmashauri
mbalimbali kwa kaya ni kati ya shilingi 5,000/= hadi shilingi 30,000/=
kwa mwaka.
Kwa wagonjwa ambao watakuwa hawana Bima ya Afya, hao watatakiwa
kuchangia gharama hiyo kwa nusu ya bei ya gharama ya dawa hizi au kwa
kiwango kingine kitakachoamuliwa na Mganga Mkuu wa Serikali kadri
itavyohitajika.
Hii ni kutokana na ukweli kwamba kung'atwa na nyoka ni ajali na wananchi
wengi wanaopatwa na ajali hii wapo maeneo ya vijijini ambao kimsingi
uwezo wao wa kumudu gharama hizi kubwa za matibabu ya dawa ya sumu ya
nyoka ni mdogo.
Wagonjwa watakaothibitika kuwa hawana fedha za kuchangia gharama hiyo,
basi hospitali husika kwa kupitia mpango wa msamaha wa kulipia huduma za
afya wahakikishe kwamba wanampatia mgonjwa huduma hizo kwa utaratibu wa
msamaha wa gharama hizo.
Aidha, kwa kuwa nchi yetu ni kubwa na ina nyoka wengi, Mhe Waziri wa
Afya anawaagiza Waganga Wakuu wa Mikoa na Halmashauri zote nchini
kupitia kwa uangalifu takwimu za wagonjwa walioumwa na nyoka katika
kipindi cha kuanzia mwaka 2013 hadi 2016 na kuziwasilisha Wizarani kabla
ya tarehe 31 Januari 2017 ili kupata takwimu za mahitaji halisi ya
dawa ya sumu ya nyoka nchini. Hii itasaidia kuboresha upangaji,
uagizaji na upatikanaji wa dawa hizo nchini.
Vile vile, Waziri wa Afya ameiagiza Bohari ya Dawa (MSD) kuweka
utaratibu wa haraka wa kununua dawa hizo moja kwa moja kutoka kwa
wazalishaji ili kupata unafuu wa bei.
Imetolewa na:-
Nsachris Mwamwaja
Mkuu Kitengo cha Mawasiliano Serikalini - Afya
26/12/2016