Na James Salvatory, BMG Dar
Shirikisho la
Wanafunzi wa Vyuo vya Elimu ya Juu nchini limemuomba Mdhibiti na Mkaguzi
Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kufanya ukaguzi wa hesabu za Sh
bilioni 1.74 za ada ya uombaji mikopo kwa mwaka huu katika Bodi ya
Mikopo (HESLB) ili kujua matumizi ya fedha hizo kwa kuwa kuna mapungufu.
Aidha,
shirikisho hilo limedai kubaini hujuma katika bodi hiyo zinazofanywa kwa
makusudi ili kuchafua utendaji wa serikali iliyopo madarakani.
Hayo yalisemwa
na Katibu Mtendaji wa shirikisho hilo, Daniel Zenda alipokuwa
anazungumzia tuhuma za hujuma hizo, akidai zinafanywa kwa makusudi ili
kurudisha nyuma jitihada njema za serikali.
Alisema ofisi
ya CAG inapaswa kufanya ukaguzi wa Sh bilioni 1.74 fedha ambazo
zilitokana na ada ya uombaji wa mikopo kwa mwaka huu ambapo kila
mwanafunzi alitoa Sh 30,000 kwa waombaji 54,000.
Alisema ni
muhimu kujua matumizi ya fedha hizo kutokana na upungufu uliojitokeza
katika upitiaji wa sifa na vigezo vya wanaostahili kupata mkopo.
Alifafanua kuwa
wanatambua hatua ya serikali katika kuhakikisha wanafunzi wenye sifa
wanapata mikopo kwa wakati ambapo takribani Sh bilioni 80 zimeongezwa
kwenye bajeti ya bodi hiyo ili kuwezesha mikopo kwa wanafunzi wote wenye
sifa.
Zenda alisema
Sh bilioni 487 zimepitishwa katika bajeti ya mwaka huu na mwaka jana
ilikuwa chini ya makadirio ya Sh bilioni 350, lakini pamoja na
kuongezeka kwa fedha hizo idadi ya wanafunzi walionufaika na mikopo
imekuwa pungufu.
“Mwaka uliopita
wanufaika wa mikopo walikuwa 53,000 na mwaka huu wanufaika wanafunzi
25,700 pamoja na ongezeko la makadirio ya zaidi ya Sh bilioni 137 kwenye
bajeti ya Mikopo bado wanafunzi wengi hawajafikiwa,” alisema.
|