NECTA YATAKA WANAOHUJUMU MITIHANI YA KIDATO CHA PILI WAFICHULIWE.

Na James Salvatory, BMG Dar
Baraza la mitihani la Tanzania (NECTA) limebainisha kwamba jumla ya watahiniwa 435,221 wameanza jana mitihani ya kidato cha pili ambapo wavulana waliosajiliwa ni 214,013 sawa na asilimia 49.17 na wasichana ni 221,208 sawa na asilimia 50.83

Jana Katibu Mtendaji Dk. Charles Msonde amesema  kuna ongezeko la asilimia 9.7 kwa watahiniwa wa mwaka huu ukilinganisha na mwaka uliopita ambapo walikuwa 396,770.

Aidha Dk. Msonde amebainisha pia jumla ya wanafunzi 1,045,999 wamesajiliwa kufanya mtihani wa darasa la nne 2016, ambapo kuna ongezeko la asilimia 0.8% ukilinganisha na mwaka uliopita.

"Maandalizi yote kwa ajili ya mitihani yamekamilika ikiwa ni pamoja na usambazwaji wa mitihani hiyo na nitoe  wito kwa wasimamizi na wanafunzi kufuata taratibu za Mitihani ikiwa pamoja na kuzingatia maadili ya taaluma.

Tunaomba wadau  wote kutoa taarifa katika vyombo husika kila wanapobaini mtu au kikundi  cha watu  kujihusisha na udanganyifu wa aina yoyote ile," alisema

Aidha aliongeza kuwa mitihani ya kidato cha pili na darasa la nne ni muhimu kwani ndio inayomuwezesha mwanafunzi kufanya mitihani yao ya mwisho ya kidato cha nne na darasa la saba.

Powered by Blogger.