MADINI YA BILIONI 3 YAKAMATWA YAKITOROSHWA VIWANJA VIKUBWA VYA NDEGE TANZANIA
Siku chache baada ya Rais John Magufuli kusema kuna utoroshaji mkubwa wa
madini kupitia viwanja vya ndege vilivyopo migodini, Wakala wa Ukaguzi
wa Madini Tanzania (TMAA) umekamata madini yenye thamani ya
Sh3,353,421,381.4 yakitoroshwa katika viwanja vikubwa vya ndege na
katika matukio 25 tofauti.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa TMAA, Mhandisi Dominic Rwekaza ameeleza hayo
katika ripoti ya ukaguzi iliyofanywa na wakala huo mwaka 2015 akisema:
“Katika kufuatilia usafirishaji wa madini nje ya nchi katika viwanja
vikubwa tulikamata madini yanayotoroshwa yenye thamani ya Dola za
Marekani 1,512,186.61 na mengine ya Sh34,670,794 katika matukio 25
tofauti.”
Akizungumza na wahariri wa vyombo vya habari nchini hivi karibuni
jijini, Rais Magufuli alisema pamoja na kwamba Tanzania ina utajiri
mkubwa wa madini, kumekuwa na utoroshwaji wa madini kwa ndege zinazoruka
kutoka kwenye baadhi ya migodi.
“Tuna dhahabu ambazo zinachimbwa, lakini utakuta watu wanasafirisha
makontena ya mchanga unapelekwa kwenda kusafishwa na sisi ndiyo
tunasindikiza na wananchi mpo mnashangilia,” alisema Rais Magufuli.
“Kwa sababu kule wanakwenda ku-separate (kutenganisha). Kwa nini
tusijenge separation plant hapa tukatengeneza ajira hapa kwa
Watanzania,” alihoji.
Viwanja vya ndege migodini
Hata hivyo, wakala huo umesema suala la migodi mikubwa kuwa na viwanja
vya ndege kwa ajili ya kusafirishia madini haliepukiki kwa sababu za
kiusalama.
Akifafanua ripoti ya ukaguzi wa madini ya mwaka 2015, Msemaji wa TMAA,
Isambe Shiwa alisema licha ya kudhibiti utoroshwaji huo viwanja vya
ndege vinatumika kusafirishia madini kutoka migodini moja kwa moja kwa
sababu za kiusalama.
“Katika maeneo yote ya madini, kuna mawakala wa ukaguzi wa madini,
wanashuhudia uzalishaji wa madini, hasa kwa dhahabu wana chukua mikuo
(mche wa dhahabu) yake na kuileta kwenye maabara zetu ili ipimwe kujua
kiasi cha dhahabu na fedha kisha wanakokotoa mrabaha kulingana na madini
husika,” alisema.
“Ili kujua faida ya madini katika mgodi husika, huwa tunafanya ukaguzi
yakinifu na kukokotoa kodi zinazotakiwa hasa kodi ya shirika. Kama kuna
utata kwenye taarifa za mgodi kuhusu ununuzi wa vifaa na mitambo,
tunakagua na kuweka wazi gharama zake kisha tunapeleka TRA kiasi
kinachotakiwa kulipwa.”
“Kwa mfano ukiangalia bei ya madini ya dhahabu, kwa wastani gramu moja
huuzwa Sh100,000, hivyo kilo moja huuzwa Sh1 bilioni.Ule mkuo mmoja una
kilo 20 hadi 25. Unaweza kuviweka vile vipande kwenye mkoba ila ni
vizito kubeba. Ukishazalisha hadi mikuo 20 ya dhahabu unabeba mabilioni
ya fedha, utasafirishaje kwa gari?
“Kuna wakati pale mgodi wa Geita (GGM) kulikuwa na ndege iliyobeba
dhahabu, kumbe tayari watu walishatoa taarifa nje kwa watu
waliojitayarisha na silaha za kivita, wakaitungua ilipokuwa ikiruka.
Bahati nzuri rubani aliimudu na kufanikiwa kuirudisha uwanjani.”
Alisema kutokana na matukio hayo, sasa wanasafirisha madini kwa
helikopta ambayo ikichukua mzigo hupaa kwenda juu zaidi kisha kwenda Dar
es Salaam ambako hukaguliwa tena kabla ya kwenda nje ya nchi.
“Kutokana na ukaguzi unaofanyika, naweza kusema hakuna madini wala
mchanga unaosafirishwa kwa wizi kwenye migodi yote.Kwanza hii migodi
inamilikiwa na wana hisa walioko ndani na nje ya nchi. Wao nao wanataka
kupata taarifa za ukaguzi wetu ili wajue wanalipa kodi kiasi gani na
wanapata nini,” alisema.
Akizungumzia sababu za madini ya tanzanite kuuzwa zaidi na Kenya, Afrika
Kusini na India, Shiwa alisema ni kutokana na Sheria ya Madini ambayo
hukata mrabaha wa asilimia tano ya madini hayo wakati sheria ya nchi
hizo haina, hivyo kuvutia zaidi wasafirisha madini kupitia nchi hiyo.
“Baada ya kugundua udhaifu huo, kamishna wetu wa madini na ofisa
mtendaji wetu mkuu walikwenda Kenya kuzungumza nao ili nao waweke
mrabaha huo na kweli waliweka. Hivyo kwa miaka minne iliyopita madini
hayo yamepungua sana Kenya,” alisema.
Alisema wamechukua pia hatua ya kuongeza thamani ya madini hayo kwa
kuyakata baada ya kujenga viwanda mkoani Arusha hivyo kupunguza
usafirishaji wa madini ghafi kupitia Kenya, Afrika Kusini na India.