Kimenuka!! AJALI YA NOAH,LORI ILIYOUA 19 SHINYANGA YANG’OA VIGOGO WA POLISI....WATUMBULIWA
Jeshi la polisi nchini kupitia kikosi cha usalama barabarani limewavua
nyadhifa zao mkuu wa kikosi cha usalama barabarani mkoa wa Tabora (RTO)
Shida Machumu, na mkuu wa usalama barabarani wa wilaya ya Nzega (DTO)
Thomas Sengecha kwa kushindwa kuwasimamia askari wa usalama barabarani
na kusababisha kutokea kwa ajali ya Noah na lori iliyoua watu 19 na
kujeruhi wawili mkoani Shinyanga.
Uamuzi huo umetolewa leo November 09,2016 na Kaimu kamanda wa kikosi
cha usalama barabarani Tanzania SACP Fortunatus Muslimu wakati akitoa
taarifa kwa vyombo vya habari mkoa wa Shinyanga kuhusu hatua
zilizochukuliwa na jeshi la polisi baada ya kutokea kwa ajali hiyo.
Ajali hiyo iliyoua watu 19 na kujeruhi watu wawili ilitokea Novemba
6,2016 katika kijiji cha Nsalala wilaya ya Shinyanga baada ya gari T232
BQR aina ya Toyota Noah iliyokuwa inatoka Nzega mkoani Tabora kwenda
Tinde mkoani Shinyanga kugongana na lori aina ya Scania lenye namba T198
CBQ likiwa na tela namba T283 CBG likitoka Tinde kwenda Nzega.
Muslimu alisema viongozi hao wanaondolewa katika nyadhifa zao kwa
kushindwa kuwasimamia askari wa usalama barabarani ambao walioondoka
katika vituo vyao vya kazi na kusababisha Noah kubeba abiria 21 badala
ya abiria wanane kama inavyotakiwa kwa mujibu wa sheria.
Kamanda Muslimu alisema baada ya kufanya uchunguzi wa kina kuhusu ajali
hiyo wamebaini kuwa inatokana na uzembe uliofanywa na askari waliokuwa
zamu kwenye kituo cha mabasi cha Nzega ambao waliondoka kituoni na
kusababisha gari aina ya Noah kubeba abiria 17,kati yao watu wazima 13
na watoto wane waliokuwa wamepakatwa na wazazi wao.
“Gari aina ya Noah ilianza safari katika kituo cha Nzega ikiwa na
abiria 17 majira ya saa 12:30 jioni...wakati gari linaondoka askari
waliopangwa kazini eneo hilo walikuwa wameshaondoka kituoni hivyo gari
hilo halikukaguliwa hivyo kutoa mwanya kwa gari hilo kubeba abiria
kupita kiasi kwa kuzidisha abiria”,alieleza Muslimu.
Alisema kitendo cha askari kuondoka eneo la tukio,kilifanya gari
izidishe abiria watano watu wazima na watoto wanne kwani Noah inapaswa
kubeba abiri wanane na si vinginevyo kwa mujibu wa sheria.
Aliongeza kuwa vile vile askari waliopangwa kazini barabarani eneo la
Uchama- Nzega nao walikuwa wameondoka eneo hilo hivyo kutoa mwanya
mwingine wa gari hilo kubeba abiria wengine wanne njiani eneo la Nata
ambapo inadaiwa kulikuwa na basi lilikuwa limeharibika na abiria
kusimamisha Noah.
“Noah ilisimama na abiria kulazimisha kupanda ndani ya gari hilo na
hivyo kuongeza idadi ya abiria katika gari hilo kufikia jumla ya watu 21
pamoja na dereva na hivyo ndani ya Noah kuwa na watu 22 na dereva
akaendesha gari kwa mwendo kasi bila kuchukua tahadhali na kasha
kugongana na lori”,alieleza Muslimu.
Alisema ajali hiyo imechangiwa na uzembe uliofanywa na askari kwa
kuondoka eneo la kituo cha Mabasi Nzega na barabarani kituo cha Buchama
hivyo mkuu wa usalama barabarani wa mkoa wa Tabora pamoja na wilaya ya
Nzega wanaondolewa katika nyadhifa zao kwa kushindwa kusimamia askari
hao.
“Tunamwondoa mkuu wa usalama barabarani wa wilaya ya Nzega Thomas
Sengecha na mkuu wa usalama barabarani mkoa wa Tabora Shida Machumu kwa
kushindwa kutekeleza mkakati wa kupunguza ajali na kushindwa kusimamia
na kuchukua hatua kwa watendaji walio chini yao kutokana na uzembe
waliofanya”,alifafanua.
Muslimu alisema wakuu hao mbali na kuvuliwa nyadhifa zao pia
wanaondolewa katika kikosi cha usalama barabarani na watapangiwa kazi
nyingine na kwamba dereva wa Noah Seif Hemed (32) mkazi wa Tinde
amefikishwa mahakamani na leseni yake tayari imeshafungiwa hataendesha
tena gari.
Aidha askari wanne waliopangwa katika kituo cha mabasi cha Nzega ambao
ni SGT Charles,E.6547 CPL Kheri,WP 6983 PC Happy na WP 7676 PC Neema na
wawili kituo cha Buchama,WP 5791 PC Cecy na WP 7165 PC Aziza
watachukulia hatua za kinidhamu na wanaondolewa moja kwa moja katika
kikosi cha usalama barabarani.
“Hatuwezi kuendelea kuona ajali zinaendelea kutokea na kupoteza maisha
ya watu kutoka na uzembe wa watendaji katika maeneo yao,hatutaki ajali
tunataka tuishi salama,”alisema Muslimu.
Aliwataka askari na viongozi kuacha kufanya kazi kwa mazoea watekeleze
majukumu yao ipaswavyo katika kuzuia ajali za abiria barabarani na
kwamba wataendelea kuchukua hatua zinazostahili kwa askari wazembe na
kuwawajibisha viongozi wote watakaoshindwa kutekeleza na kusimamia
majukumu yao.
Na Kadama Malunde- Malunde1 blog