RAIS MAGUFULI AMPONGEZA DONALD TRUMP


RAIS John Magufuli amemtumia salamu za pongezi Rais mteule wa Marekani, Donald Trump ambaye jana aliibuka mshindi wa Uchaguzi Mkuu wa nchi hiyo, uliofanyika juzi na hivyo kumfanya kuwa Rais wa 45 wa taifa hilo kubwa lenye nguvu kubwa ya kiuchumi na kijeshi.
Katika salamu zake kupitia anuani yake ya mtandao wa Tweeter, Dk Magufuli aliandika, “Hongera Rais mteule Donald Trump na watu wa Marekani. Mimi na Watanzania tunakuhakikishia kuendeleza urafiki na ushirikiano wetu.”
Tanzania imekuwa mshirika mkubwa wa Marekani kwa miaka mingi na katika siku za karibuni, Tanzania imenufaika na misaada ya mabilioni ya shilingi katika sekta za elimu, afya, maji, miundombinu ya barabara na nishati ya umeme.
Bungeni Dodoma, Naibu Spika, Dk Tulia Ackson amempongeza mgombea huyo wa chama cha Republican, Trump kwa kushinda nafasi hiyo na kuwa rais mpya wa Marekani.
Aidha, Dk Ackson amesema yeye binafsi na wabunge wengine wanawake, wamesikitishwa na kushindwa kwa mgombea urais wa Democrat, Hillary Clinton.
Naibu Spika aliyasema hayo jana bungeni baada ya kipindi cha maswali na majibu, wakati akitambulisha wageni. Alisema walitarajia kwamba mambo yangekuwa mazuri kwa upande wao (wanawake), lakini haikuwezekana.
“Nachukua nafasi hii kumpongeza Trump kushinda uchaguzi wa Marekani, Hillary hakuweza labda baada ya miaka minne ijayo. Tunatambua juhudi zake na amejitahidi sana,” alisema Dk Tulia huku akishangiliwa na wabunge wengi wakiwa wanawake. Akifanya utani, Dk Tulia alisema, “Nasikia kuna watu hapa wanasema tungempeleka mheshimiwa fulani… katika maeneo yale mama Clinton angeshinda,” alisema na kushangaliwa.
Awali, wakati wa kipindi cha maswali jana, Mbunge wa Viti Maalumu, Suzan Lyimo (Chadema) alisema ana masikitiko makubwa kwa sababu Hillary ameshindwa.
“Kwa niaba ya wanawake wenzangu nampa pole Mama Clinton. Tumeumia na tumerudi nyuma,” alisema Lyimo na Naibu Spika alimuuliza amepata wapi hiyo taarifa wakati walikuwa na matumaini Hillary angeshinda.
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Hamis Kigwangalla akijibu swali la Lyimo, alimpa pole Hillary kwa kushindwa katika uchaguzi huo.
Alisema yeye ni Balozi wa Wanawake, anawapenda wanawake na kwa sababu hiyo anampa pole mgombea huyo wa Democrat kwa kushindwa na anampongeza Trump kwa ushindi. Wamarekani walipiga kura juzi kumchagua raia atakayemrithi rais wa sasa, Barack Obama.
Trump aweka rekodi
Kinyume cha matarajio ya wengi, bilionea Donald Trump ameibuka mshindi katika kinyang’anyiro cha urais wa Marekani kilichokuwa na ushindani mkali, akiweka rekodi ya kuwa rais mwenye umri mkubwa zaidi kuwahi kushinda urais. Juni 14 mwaka huu, Trump alitimiza umri wa miaka 70.
Kabla yake, Ronald Reagan alishinda uchaguzi akiwa na umri wa miaka 69 mwaka 1980. Trump, aliyeoa mara tatu, huku akiacha wake wawili, Ivana Zelnickova (1977 -1991) na Marla Maples na (1993 - 1999) na kisha mwaka 2005 kumuoa Melania Knauss anayeingia naye Ikulu, ni baba wa watoto watano, Donald Jr, Ivanka, Eric, Tiffany na Barron.
Ni bilionea msomi wa uchumi kutoka Chuo Kikuu cha Pennyslania, aliyepaisha utajiri wa familia yao, kutokana na kuwekeza katika biashara mbalimbali zikiwemo za majengo, hoteli za kifahari na aina nyingine za biashara ambazo tathimini ya Forbes mwaka huu ilimweka katika nafasi ya bilionea namba 156 Marekani, akiwa wa 324 duniani kutokana na utajiri unaokadiriwa kuwa wa dola bilioni 9 (sh trilioni 19).
Kwa kutambua umuhimu wa elimu, yeye mwenyewe ni mmiliki wa Chuo Kikuu cha Trump kinachotoza ada nafuu. Anamiliki pia jengo la ghorofa 58 katika jiji la Manhattan, achilia mbali majengo mengine ya kifahari katika sehemu mbalimbali za Marekani.
Katika kujichanganya kibiashara, aliwekeza pia katika michezo na sekta ya burudani akiwa mmiliki wa kampuni iliyoandaa mashindano ya Miss Universe, Miss USA, Teen USA kati ya mwaka 1996 na 2015.
Kuna wakati alisimamia pia mapambano ya bondia mashuhuri Mike `Iron’ Tyson, kabla ya kuachana naye baada ya bondia kukumbwa na kashfa ya kubaka na kutupwa gerezani, ingawa aliendelea kuwa rafiki yake.
Aliwekeza pia katika fani ya mitindo, akiwa na kampuni kubwa lakini pia ni shabiki mkubwa wa filamu, huku yeye mwenyewe akishiriki kucheza baadhi na kuingiza fedha. Miongoni mwa filamu alizohusika nazo ni vichekesho ya Home Alone 2 ya mwaka 1992.
Nyingine na miaka yake kwenye mabano ni Ghosts Can’t Do It (1989), Across the Sea of Time (1995), The Little Rascals (1995), Eddie (1996), The Associate (1996) Celebrity (1998), Zoolander (2001), Two Weeks Notice (2002) na Wall Street: Money Never Sleeps ya mwaka 2010.
Alianza kujipambanua upande wa siasa mwaka 1987 akiwa na Republican, alishauri na kusaidia mambo kadhaa, ikiwa ni pamoja na kampeni. Mwaka 2000 alijaribu kupima maji katika uongozi, lakini akaishia njiani.
Lakini kufikia mwaka 2013, aliamua kutumia dola milioni moja (Sh bilioni 2.1) za Marekani kutafiti kama anaweza kujipenyeza na kuwania urais wa Marekani. Na baada ya kujiridhisha, ndiko akakusanya nguvu na kuingia rasmi katika `vita’ ya kuusaka urais.
Wakati anatangaza dhamira yake Juni mwaka jana, wengi walimbeza, lakini alipambana na kuibuka mtu muhimu katika karata za kisiasa ndani ya chama hicho, huku wapinzani wake wakianguka mmoja baada ya mwingine. Ilipofika Julai mwaka huu alitangazwa rasmi kuwa mgombea wa urais kwa tiketi ya Republican.
Kuanzia hapo, alikumbana na upinzani, vikwazo na suluba za kila aina za kisiasa, kiasi cha kuwakatisha tamaa baadhi ya washirika wake wakiwemo pia viongozi wa juu wa chama, ambapo baadhi walijiengua katika kampeni zake. Lakini, alisimama imara na kuamua kupambana mithili ya `jeshi la mtu mmoja’.
Chanzo-Habarileo
Powered by Blogger.