Na James Salvatory, BMG Dar
Dawa bandia
zisizofaa kwa matumizi ya binadamu zimekamatwa katika baadhi ya maeneo
ya Kanda ya Ziwa na Nyanda za Juu Kusini baada ya ukaguzi maalum wa
kusaka dawa bandia uliofanywa na Mamlaka ya Chakula na Dawa nchini
(TFDA).
Mkurugenzi Mkuu
wa Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) Hiiti Sillo ametanabaisha hayo
wakati akitoa taifa ya matokeo ya ukaguzi maalum wa dawa uliofanyika
katika mikoa ya Kanda ya Ziwa na Nyanda za Juu Kusini.
“Kutokana na
ukaguzi maalum tulioufanya katika Kanda hizo kutafuta dawa bandia na
zisizo sahihi kwa matumizi ya binadamu tumefanikiwa kukamata dawa bandia
aina tano ambazo zipo kwenye makundi mawili ya Dawa za malaria na Viua
vijasumu(Antibiotics)” alisema
Aidha Sillo
alisema kuwa ukaguzi huo maalum umeweza kusaidia kukamata dawa ya
malaria aina ya vidonge vya Quinine ambayo inadaiwa kutengenezwa katika
kiwanda cha Elys Chemical nchini Kenya na nyingine zinatengenezwa hapa
nchini katika kiwanda cha Shelys Phamaceuticals Ltd.
Alisema kuwa
pamoja na kukamata dawa bandia pia zoezi hilo lilifanikiwa kubaini na
kukamata dawa zilizoisha muda wa matumizi , zisizosajiliwa zenye ubora
duni zenye thamani ya Tsh. Milioni 17.463.
Aliongeza kuwa
Ukaguzi huo ulitokana na kuwa na taarifa za awali ambazo zilionyesha
uwepo wa dawa bandia katika maeneo ya Geita na Mara mwezi Agosti na
Septemba mwaka huu na kusistiza kwamba zoezi hilo la ukaguzi linaendelea
nchini kote na watakaokutwa na hatia watachukuliwa hatua stahiki.
Kwa upande wake
Msajili wa Baraza la Famasia Elizabeth Shekalaghe, alisema kuwa
wataalamu wa madawa watakaokutwa na hatia ya kusambaza na kuhudumia dawa
bandia watafutiwa usajili na kuacha kutoa huduma kwa mujibu wa sheria
ya dawa , chakula na vipodozi.
“Wataalamu wa
dawa ambao wanasambaza na kuhudumia dawa bandia watafutiwa usajili na
kuacha kutoa huduma kwa mujibu wa sheria ya dawa , chakula na vipodozi
pindi watapogundulika” alisema Bi. Shekalaghe.
Pamoja na hayo
alisema kuwa ukaguzi huo ulianza Oktoba 4 mwaka huu na unafanywa kwa
ushirikiano wa TFDA, Jeshi la polisi na Maafisa kutoka Baraza la Famasia
Tanzania na litakuwa endelevu.
|