MKOA WA SIMIYU KUJIKITA NA UTENGENEZAJI WA BIDHAA ZA NGOZI.
Judith Ferdinand, Mwanza
Mkoa wa Simiyu
utajikita katika uwekezaji na utengenezaji wa bidhaa mbalimbali
hususani za ngozi ikiwemo mipira kwa ajili ya kuuza na kuwasaidia
wajasiriamali wadogo na kati kujiinua kiuchumi.
Hayo yalisemwa
juzi na Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Anthony Mtaka alipotembelea Shirika la
Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO)Mwanza na Taasisi ya Teknolojia ya Dar es
Salaam (DIT) tawi la Mwanza, kwa ajili ya kujionea shughuli
zinazofanywa,ili kujifunza na kuyafanyia kazi kwa vitendo katika mkoa
wake, ikiwa ni juhudi za ushawishi wa Meneja wa SIDO Damian Chang'a
wakati alipomtembelea mkoani kwake hivi karibuni.
Mtaka mara
baada ya kutembelea na kujionea shughuli zinazifanywa na kiwanda cha
Mwanza Quality Wines kilichopo ndani ya SIDO, aliahidi kuanzisha kiwanda
kama hicho mkoani Simiyu ambacho kitatumia malighafi tofauti, ili
kuingia katika soko la ushindani.
Aidha aliahidi,
kuanzisha kiwanda kwa ajili ya bidhaa za ngozi na watajikita zaidi
katika utengenezaji wa mipira ili kuinua uchumi wa mkoa na wajasiriamali
mkoani humo, hii ni baada ya kukagua na kujionea namna DIT
wanavyotengeneza na kuzalisha bidhaa kwa kutumia ngozi za wanyama.
Kwa upande wake
Chang' a alisema, SIDO ipo kwa ajili ya kuwezesha wajasiriamali wadogo
na wa kati pamoja na viwanda vidogo na vya kati,pia wanamatawi katika
mikoa ya Tanzania Bara isipokuwa mkoa wa Simiyu na Songwe, hivyo
alitumia fursa hiyo kumshawishi Mtaka kutembelea shirika na taasisi
hiyo ili kujionea shughuli zinazofanyika.
Vilevile
alisema, shirika hilo tangu kuanzishwa kwake, limeweza kutoa mafunzo ya
stadi mbalimbali kwa wajasiriamali, ambao wengi wao wamefanikiwa na
kuweza kujiinua kiuchumi na kujiajiri na kuajiri wengine, ambapo
alitolea mfano kiwanda cha Mwanza Quality Wine ambapo mmiliki wake
ametokea mikononi mwa SIDO huku akianza na mtaji wa 500,000 na mpaka
sasa anamtaji wa sh bilioni moja.
Naye Mkurugenzi
wa Mwanza Quality Wines Leopord Lema aliwaomba, wajasiriamali
kutokukata tamaa bali waendane na hali ya biashara,mpaka sasa ni miaka 9
tangu kuanzia kiwanda hicho na alianza na mtaji wa laki tano ila sasa
anamtaji wa bilioni moja pamoja na kuajiri wafanyakazi 24.
Aidha alisema, lengo lake baaada ya miaka 3, akipata eneo atajenga kiwanda kikubwa nchini kitakachozalisha wine.
Kadhalika Mkuu
wa Chuo cha DIT Albert Mmari alisema, taaluma wanayotoa ni yakuwezesha
viwanda vidogo kuanzia ngazi ya familia, vijiji,wilaya mpaka taifa,hivyo
mkoa wa Simiyu pia unaweza kutengeneza mipira na watoto wakaacha
kuchezea ya makaratasi.
