|
Serikali
imeshauriwa kutoa ushirikiano kwa watetezi wa haki za binadamu ili kurahisisha
utendaji kazi wao badala ya kuwaona watetezi hao kama wachochezi katika jamii
na wakati mwingine kuwafungulia mashitaka.
Ushauri
huo umetolewa hii leo Jijini Mwanza na Mratibu wa Taifa wa Mtandao wa Watetezi
wa Haki za Binadamu nchini, Onesmo Olengurumwa, kwenye mafunzo ya siku tatu kwa
watetezi wa haki za binadamu kutoka mikoa mbalimbali nchini.
Amesema
katika baadhi ya maeneo kama Loliondo mkoani Arusha kwenye mgogoro wa ardhi
kati ya wananchi na mwekezaji, watetezi wa haki za binadamu wamechukuliwa kama
wachochezi na kufunguliwa mashitaka jambo linalosababisha baadhi yao kushindwa
kutekeleza majukumu yao na wengine kuacha kabisa shughuli za utetezi.
Akifungua
Mafunzo hayo, Kaimu Kamishna Msaidizi wa Madini Kanda ya Ziwa Victoria
magharibi, Mayigi Makobela, amesema serikali itaendelea kuwaelimisha wachimbaji
wadogo ili waifahamu vyema sheria ya madini namba 4 ya mwaka 2010 ili kupunguza
migogoro iliyopo na kwamba imetenga zaidi ya hekta elfu 12 kwa ajili ya
wachimbaji wadogo wadogo wa madini.
Pia
amesema serikali imetenga shilingi bilioni 6.6 kwa ajili ya ruzuku kwa
wachimbaji wadogo na kuwahimiza kujiunga kwenye vikundi ili wapatiwe ruzuku
hiyo.
Baadhi
ya washiriki wamesema mafunzo hayo yatawasaidia kuimarisha utendaji wao wa kazi
jambo litakalowasaidia kutimiza vyema wajibu wao katika jamii
|