Wabunge wa
upinzani wameendelea kususia kwa siku ya tatu mfululizo vikao vya Bunge
vinavyoendeshwa na Naibu Spika, Dkt. Tulia Ackson tangu walipotangaza hatua
hiyo Jumatatu wiki hii kwa kutokuwa na imani naye.
Tangu Jumanne wiki hii wabunge
hao wamekuwa wakisusa vikao vinavyoongozwa na kiongozi huyo kwa madai kuwa
anaminya demokrasia.
Siku hiyo wabunge hao waliingia
bungeni kama kawaida na Dk Tulia alipomaliza tu kusoma dua ya kuliombea Bunge,
walitoka hadi kipindi hicho kilipomalizika na naibu spika kumwachia mwenyekiti
wa Bunge, Andrew Chenge kuongoza, ndipo wote waliporudi ukumbini na kuendelea
na shu ghuli zao kama kawaida.
Juzi, wabunge hao wote kama
kawaida waliingia bungeni asubuhi na alipoingia Dk Tulia kuongoza kikao hicho,
walisimama na kusikiliza dua ya kuliombea Bunge, kisha walitoka na kuwaacha
wabunge wa CCM wakiendelea na Bunge.
Siku nzima ya juzi ambayo Dk
Tulia aliendesha kikao cha asubuhi na jioni, wabunge hao hawakuhudhuria na
ilipofika wakati wa kusoma hotuba ya msemaji wa kambi ya upinzani kwa Wizara ya
Fedha na Mipango, David Silinde aliingia ukumbini akitokea nje na kuomba hotuba
yake iingie kwenye kumbukumbu rasmi za Bunge kama ilivyo. Kisha akasema:
“Sitaisoma hapa kwa kuwa haturidhishwi na mwenendo wa Naibu Spika wa
kutuendesha kama watoto.”
Wabunge hao wa upinzani walitoa
sababu sita kwanini wanataka Dk Tulia aondolewe madarakani kwa Azimio la Bunge.
Akizungumza na waandishi wa
habari jana kwa niaba ya wabunge hao, Mbunge wa Simanjiro, James Millya
alizitaja sababu hizo kuwa ni kwanza Dk Tulia ameweka maslahi ya chama chake
cha siasa mbele kuliko maslahi ya Bunge, kinyume na Kanuni ya 8(b) ya Bunge.
“Pili, Mei 6 alitumia vibaya
madaraka ya kiti cha Spika kwa kutoa uamuzi wa mwongozo ambao ulikuwa unakiuka
Ibara ya 12(2) ya Katiba. Muongozo huo uliokuwa unapinga udhalilishaji wa
wabunge wanawake,” alisema.
Ya tatu ni kitendo cha Dk Tulia
kuvunja Kanuni ya 64(1) (f) na (g) zinazokataza mbunge kutumia lugha ya matusi
kwa mbunge mwingine ambapo alinukuliwa akisema “Mheshimiwa Bwege, usionyeshe
ubwege wako humu ndani.”
Alisema ya nne ni Mei 30
kiongozi huyo aliamua kwa makusudi kuvunja Ibara ya 63(2) ya Katiba na kutumia
vibaya Kanuni ya 69(2) na 47(4) ya Kanuni za Bunge kumzuia Joshua Nassari kwa
upande mmoja na Bunge zima kwa upande wa pili kutimiza majukumu yake ya
kikatiba ya kusimamia na kuishauri Serikali.
“Sababu ya tano ni kuwa Mei 26,
mwaka huu Dk Ackson akiongoza kikao cha Bunge bila ridhaa ya upinzani
alishiriki kufuta sehemu ya hotuba ya msemaji wa upinzani kwa Wizara ya Elimu,
Sayansi na Teknolojia kinyume cha kanuni ya 99(9) ya Bunge bila kushirikisha
kamati yoyote ya Bunge,” alisema.
|