KESI ya madai iliofunguliwa na Freeman
Mbowe, Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(Chadema) ya kuiomba mahakama kupiga marufuku zuio la Polisi, leo
limetupiliwa mbali.
Mbowe alifungua kesi hiyo namba 79 ya mwaka 2016, baada ya hivi
karibuni Jeshi la Polisi kupiga marufuku mikutano ya hadhara kwa madai
kwamba, hali ya usalama nchini si salama.
Mbowe ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Hai, Kilimanjaro katika shauri
hilo, aliwashtaki Mkuu wa Polisi Wilaya ya Geita na Mwanasheria Mkuu wa
Serikali (AG), kwa madai wanahusika kuzuia kufanyika kwa mikutano ya
hadhara ya vyama vya siasa.
Mbowe ni Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani bungeni, walitangaza
kufanya oparesheni iliyopewa jina ‘Okoa Demokrasia nchini’ iliyokuwa na
lengo la kuishtaki serikali kwa wananchi kwa kile alichodai, kuendesha
nchi bila kufuata katiba ya nchi.
Hata hivyo, baada ya kupigwa marufuku kwa maandamano, Mbowe alifungua
kesi ya madai katika Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Mwanza, akiiomba
kutengua zuio hilo la polisi.
Mohammed Gwae, Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Mwanza, leo
amepitia ombi lililopelekwa mahakamani hapo na upande wa mlalamikaji
anayewakilishwa na mawakili John Mallya na Gasper Mwanalelya na kutoa
uamzi.
Jaji Gwae akitoa uamuzi wa ombi la walalamikaji amedai kuwa, amefikia
hatua hiyo baada ya walalamikaji kukosea kifungu cha kupeleka shauri
hilo kortini kitendo kilichosababisha kulitupilia mbali.
Amesema kuwa, walalamikaji baada ya kupeleka ombi hilo kortini, upande
wa wajibu maombi unaoongozwa na mawakili, Seth Mkemwa na Robert Kidando
waliweka pingamizi wakiomba mahakama kutokusikiliza ombi hilo.
Jaji Gwae amesema kuwa, walalamikaji katika ombi lao walikosea kutumia
kanuni ya tano kifungu kidogo cha tatu cha sheria ya mwaka 2014 badala
ya kanuni ya tano kifungu kidogo cha pili ambacho kilitakiwa kutumiwa.
“Waleta maombi wametumia kanuni ya tano kifungu kidogo cha tatu badala
ya kutumia kanuni ya tano kifungu kidogo cha pili kilichotakiwa kuwepo
katika kuleta ombi na kama kifungu hiki hakijatumika hapo na ombi
halipaswi kupokelewa,” amesema Jaji Gwae.
Hata hivyo Jaji Gwae amesema, licha ya kuwekewa pingamizi na wajibu
maombi, walalamikaji wamesema kanuni na kifungu hicho ndivyo vilitakiwa
kuwepo na hivyo vinavyopaswa kuwekwa sio sahihi.
Amesema kuwa, katika shauri la namna hiyo, kanuni na vifungu
vilivyotakiwa kuwepo ni kanuni ya tano kifungu kidogo cha pili na kanuni
ya tano na kifungu kidogo cha sheria ya mwaka 2014 na kwamba wao
waliviweka katika maelezo (Statements) badala ya (chember samers).
Mallya, mwanasheria wa mpeleka maombi amesema kuwa, baada ya kukosea
kanuni na vifungu hivyo, watapeleka kwa mara nyingine ombi na kulifanyia
marekebisho kama Jaji Mohamed Gwae alivyoelekeza. |