Serikali ya Tanzania imepitisha
bajeti ya shilingi trilion 29.5 kwa kupigiwa kura huku wabunge wa upinzani
wakiwa wametoka nje wakiwa wameziba midomo yao kwa karatasi na plasta ikiwa ni
ishara ya kuonesha kutoridhika na Naibu Spika Dkt. Tulia Ackson wakigomea vikao
vya Bunge vinavyoongozwa na Naibu Spika huyo
Katika vikao vya Bunge la 11,
wabunge wa vyama vya upinzani wamekuwa wakisusia vikao hivyo kwa takribani siku
23 sasa kwa madai ya kutokubaliana na ukandamizaji unaofanywa na Naibu Spika wa
Bunge Dkt.Ackson Tulia.
Wakichangia bajeti hiyo, Waziri
wa Nishati na Madini Prof Sospeter Mwijarubi Muhongo pamoja na Waziri wa Viwanda
na Biashara Charles Mwijage wamesema bajeti hiyo inalenga kukuza uzalishaji.
Akijibu hoja mbalimbali za
wabunge waliochangia katika Bajeti hiyo ikiwa ni pamoja na ya kuongeza fedha
katika ofisi ya mkaguzi wa serikali CAG ili kutanua wigo wa ukaguzi pamoja na
kuachana na mpango wa kuanza kuwakata kodi wabunge katika mafao ya kiinua
mgongo ya Wabunge, Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Phillip Mpango amesema
msimamo wa serikali upo pale pale.
Kuhusiana na makato ya kodi
kwenye mafao ya wabunge, Dkt Mpango amesema kuwa serikali imeamua kuwa itakata
kodi hiyo kwa viongozi wote wa kisiasa wakiwemo wakuu wa wilaya, wakuu wa mkoa,
Waziri Mkuu, Makamu wa Rais na Rais pia, ili kuweka usawa katika makato ya kodi
nchini.
Baadaye jioni wabunge walipiga
kura mmoja mmoja kupitisha bajeti hiyo, ambapo wabunge wote 251 waliokuwemo
bungeni walipitisha bajeti hiyo kwa kauli moja, ambapo kila mbunge alijibu
"Ndiyo" akimaanisha anaipitisha bajeti hiyo.
Mapema Asubuhi mara baada ya
dua, wabunge wa upinzani waliziba midomo yao kwa karatasi na Plasta na kutoka
nje ya ukumbi wa Bunge ikiwa ni ishara ya kuonesha kutoridhika na Naibu Spika
wa Bunge Dkt. Tulia Ackson.
Mbunge wa Vunjo Kupitia chama
cha NCCR Mageuzi, Mhe. James Mbatia kwa niaba ya wabunge hao alisema hawataacha
kulalamikia ukiukwaji wa sheria unaofanywa na kiti cha Naibu Spika.
|